Iran yazima mashambulio ya droni katika mkoa wa Isfahan
Wizara ya Ulinzi ya Iran imesema vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu vimefanikiwa kuzima mashambulio ya ndege zisizo na rubani (drone) dhidi ya kituo cha kijeshi katika mji wa Isfahan, katikati mwa nchi.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Wizara ya Ulinzi ya Iran imeeleza kuwa, moja ya droni hizo (MAVs) ilishushwa chini na mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran katika mashambulio hayo ya jana Jumamosi usiku, huku nyingine mbili zikitunguliwa.
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, mashambulio hayo yaliyofeli hayakusababisha maafa ya binadamu, lakini yameharibu paa la kiwanda hicho kwa kiasi kidogo. Hata hivyo, taarifa hiyo imeeleza, shughuli zinaendelea katika kampuni hiyo ya kuzalisha zana za kijeshi.
Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeeleza bayana kuwa, mashambulio 'pofu' ya aina hiyo hayatakuwa na taathira yoyote kwa hatua za ustawi na maendeleo za taifa hili la Kiislamu.
Imesema vyombo vya usalama na ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu vimefanikiwa kuzima mashambulio hayo katika mji wa Isfahan, katikati mwa nchi kutokana na kuwa kwao macho.
Ikumbukwe kuwa, Novemba mwaka uliomalizika, watu watatu waliuawa huku askari usalama wanane wakijeruhiwa wakati wa ghasia huko Semirom katika mkoa wa Isfahan katikati mwa nchi.
Aidha askari wawili wa usalama pia waliuawa shahidi na magaidi na wengine wawili walijeruhiwa katika mji wa Malekshahr katika mkoa huo huo wa Isfahan.