Amir-Abdollahian: Uhusiano wa Iran na Guinea unazidi kuimarika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i93858-amir_abdollahian_uhusiano_wa_iran_na_guinea_unazidi_kuimarika
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Guinea ni mzuri, wa kirafiki, wa kihistoria na unaoendelea kuimarika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2023 08:42 UTC
  • Amir-Abdollahian: Uhusiano wa Iran na Guinea unazidi kuimarika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Guinea ni mzuri, wa kirafiki, wa kihistoria na unaoendelea kuimarika.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na Waziri wa Utamaduni, Utalii na Sanaa wa Guinea, Alpha Soumah, ambaye yuko safarini hapa Iran na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa nchi mbili hizi kuendelea kubadilishana jumbe mbalimbali. 

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, kufanyika vikao vya mara kwa mara vya kamisheni za pamoja za Iran na Guinea kutapiga jeki mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi baina ya mataifa haya mawili.

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Utalii na Sanaa wa Guinea, Alpha Soumah amesisitizia ulazima wa kuimarishwa ushirikiano wa pamoja wa Iran na Guinea katika nyuga mbalimbali.

Soumah ametoa mwito wa kuchukuliwa hatua za kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili hizi katika nyuga tofauti, akisema kuwa anatumai taifa lake la Afrika Magharibi litastafidi na uzoefu wa Iran katika miradi ya maendeleo.

Kuimarika uhusiano wa Iran na bara Afrika

Kadhalika Waziri wa Utamaduni, Utalii na Sanaa wa Guinea amesema anatazamia kuwa kikao cha kamisheni za pamoja za Iran na Guinea kitafanyika katika mustakabali wa karibu.

Mawaziri hao wawili wa Iran na Guinea wamejadiliana pia masuala yenye maslahi na maendeleo ya ushirikiano wa pamoja, haswa katika nyuga za siasa, utamaduni, sayansi na uchumi.