Nchi 90 zinataka kupokea ndege zisizo na rubani (droni) za Iran
Mshauri wa Waziri wa Intelijensia wa Iran amesema nchi zipatazo 90 duniani zina hamu ya kupokea ndege zisizo na rubani (droni) za Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr, Mshauri wa Waziri wa Intelijensia wa Iran ambaye pia anaongoza taasisi ya wanafikra wa kisiasa katika wizara hiyo amesema, nchi za Magharibi zinashindwa kustahamili ukweli kwamba, mataifa 90 duniani yana hamu kubwa ya kumiliki droni 90 za Iran.
Amesema hii leo na licha ya vikwazo shadidi na mashinikizo ya maadui, uwezo mkubwa wa kiulinzi wa Iran katika eneo la Asia Magharibi unawatia kiwewe Wamagharibi wakiongozwa na Marekani, na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Katika miaka ya hivi karibuni Iran imepiga hatua kubwa za mtawalia katika kubuni, kutengeneza na kuzalisha ndege zisizo na rubani za kijeshi na kuzipeleka katika nchi zilizoko nje ya ukanda wa Mashariki ya Kati.
Hivi karibuni, Brigedia Jenerali Hamid Vahedi Kamanda wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajitosheleza katika uundaji wa ndege zisizo na rubani (droni).
Jeshi la Anga la Iran karibuni liliunda droni mbili za kimkakati na za thamani kubwa kwa majina ya Kaman 12 na Kaman 22. Aidha Wizara ya Ulinzi ya Iran imeunda ndege nyingine kadhaa zisizo na rubani.
Sekta ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu imekuwa na mafanikio mbalimbali nchini katika nyanja tofauti za nchi kavu, baharini, anga, na makombora.
Julai mwaka jana, gazeti la The New York Times la Marekani liliwanukuu wataalamu mbalimbali wakisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa msafirishaji nje mkubwa wa droni duniani na inazidi kueneza ushawishi wake katika maeneo tofauti ya hata nje ya Asia Magharibi.