Iran: Kundi la 5+1 lazima litekeleza makubaliano ya Vienna
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelitaka kundi la 5+1 kutekeleza barabara makubaliano ya nyuklia kati ya Tehran na madola 6 yenye nguvu duniani yaliyofikiwa huko Vienna Julai mwaka jana.
Katika mazungumzo na Didier Burkhalter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi mjini Bern, Majid Takht-e Ravanchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran imetekeleza upande wake wa makubaliano hayo na kwa msingi huo upande wa pili unapaswa kutekeleza wajibu wake.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi amesema serikali ya Bern iko tayari kuimarisha ushirikiano wake na Tehran katika nyuga tofauti haswa baada ya makubaliao hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Amesema Usiwisi iko tayari kuimarisha uhusiano wake na Iran katika nyuga za elimu, uchumi na utafiti.
Iran mara kadhaa imesisitiza kuwa vikwazo vya kiuchumi, kifedha na kibenki, viwe ni vile vilivyowekwa na Baraza la Usalama au vile vilivyowekwa na Kongresi ya Marekani au vile vilivyowekwa na serikali ya Marekani, lazima vyote viondolewe baada ya kutiwa saini makubaliano hayo. Hata hivyo Marekani imekuwa ikiweka vizingiti katika uondolewaji wa vikwazo hivyo kinyume ncha mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani.