Haki za binadamu ni mhanga wa siasa za nchi za Magharibi
Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ambaye pia ni Katibu wa Idara ya Masuala ya Haki za Binadamu ya Iran, amesema siasa zinadhuru pakubwa suala zima la haki za binadamu na kuongeza kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuheshimu misingi ya tasnia ya uandishi habari na kubainisha ukweli wa mambo mbali kabisa na mifungamano ya kisiasa.
Akizungumza jana Alkhamisi mbele ya waandishi wa vyombo vya habari vya kigeni kuhusu suala la haki za binadamu kuwa la kimataifa, Kazem Gharibabadi, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Kimataifa na Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu ya Vyombo vya Mahakama vya Iran ametaja siasa kuwa janga la haki za binadamu na kuongeza kuwa: Haki za binadamu zimefanywa kuwa mhanga wa siasa. Ametolea mfano ukweli huo watu wa Yemen na kusema kwamba inasikitisha kuona kuwa watu hao masikini na wasio na hatia wamenyimwa haki zao zote za msingi ikiwa ni pamoja na fursa ya kupewa misaada ya kibinadamu.
Gharibabadi amesema: Siaza za haki za binadamu za Iran zimejikita katika msingi wa kuunga mkono na kuimarisha haki za binadamu katika ngazi za ndani na kuboresha maingiliano na ushirikiano wa kimantiki na wa kuheshimiana na taasisi za kimataifa za haki za binadamu.
Huku akiashiria kuwa wadai wa uongo wa haki za binadamu wamenyamazia kimya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani ambavyo vinatekelezwa na serikali za Ulaya na hivyo kuathiri maisha ya mamilioni ya Wairani, Gharibabadi amesema watu wa Iran ni wahanga wakuu wa vitendo vya magaidi wanaodhaminiwa na nchi za Magharibi ambapo Wairani wasio na hatia wapatao 17,000 wamepoteza maisha kutokana na vitendo hivyo.

Gharibabadi amesema, maadui wanatumia nguvu na uwezo wao wote kueneza propaganda na uongo dhidi ya Iran kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Amesema vyombo vya habari vinapaswa kutekeleza majukumu yao kitaalamu na kitasnia na kujiepusha na siasa pamoja na propaganda haribifu za baadhi ya nchi dhidi ya Iran.
Mwishoni mwa mwezi Septemba, baadhi ya mikoa ya Iran ilishuhudia machafuko, na katika siku za kwanza kabisa, baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni vilikuwa na nafasi kubwa katika kueneza ghasia hizo.
Katika machafuko hayo, viongozi wa Marekani, utawala wa kibaguzi wa Israel na baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na vyombo vyao vya habari na vingine vinavyotangaza kwa lugha ya Kifarsi vinavyodhaminiwa na nchi hizo za Magharibi, vilikuwa na mchango mkubwa katika kuchochea ghasia hizo zilizohatarisha pakubwa usalama wa taifa la Iran kwa kisingizio cha eti kuunga mkono haki za watu wa Iran.
Juhudi hizo za kichochezi na za mara kwa mara zinazofanywa na nchi za Magharibi na vyombo vyao vya habari zimekuwa zikikabiliwa na matembezi na maandamano ya mamilioni ya wananchi wa Iran wanaojitokeza kwa umati mitaani na viwanjani kutetea na kuunga mkono mfumo wa Kiislamu na kimapinduzi unaotawala nchini.