Waislamu nchini Iran, duniani washerehekea Idul Fitr
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96542-waislamu_nchini_iran_duniani_washerehekea_idul_fitr
Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine nyingi kote duniani leo wanasherehekea siku kuu ya Idul Fitr kuashiria kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, baada ya kuandama mwezi mpya wa mwezi wa Shawwal jana Ijumaa jioni.
(last modified 2026-07-03T11:45:53+00:00 )
Apr 22, 2023 02:44 UTC
  • Waislamu nchini Iran, duniani washerehekea  Idul Fitr

Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine nyingi kote duniani leo wanasherehekea siku kuu ya Idul Fitr kuashiria kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, baada ya kuandama mwezi mpya wa mwezi wa Shawwal jana Ijumaa jioni.

Katika mji mkuu wa Iran, Tehran, makumi ya maelfu ya waumini walikusanyika kwenye uwanja wa Sala wa Imam Imam Khomeini (MA)  kuswali Sala ya Idul Fitr. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyed Ali Khamenei alisalisha Sala hiyo.

Baadhi ya nchi za Kiislamu zikiwemo Saudi Arabia, Qatar, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, Yemen, Palestina, Syria na Misri zilitangaza kuwa siku ya jana Ijumaa kuwa tarehe Mosi Shawwal.

Aidha nchi kadhaa za Kiislamu zikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Oman, Pakistan, Indonesia, Malaysia pamoja na Iraq zimetakngaza leo kuwa siku ya kwanza ya Shawwal na hivyo sherehe za Idul Fitr zimeanza leo katika nchi hizo kwa sala maalumu ya siku hii. Katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania, idadi kubwa ya Waislamu pia wameanza sherehe za Idul Fitr hii leo ingawa kuna makundi yaliyoanza maadhimisho yao hiyo jana.

Wakati huo huo,  Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za pongezi  kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu kwam nasaba wa kuwadia sikukuu ya Idul Fitr kutuma ujumbe tofauti.

Sala ya Idul Fitr katika Haram Takatifu ya Imam Ridha AS kaskazini mashariki mwa Iran

Kwa mujibu wa Kurugenzi Kuu ya Habari ya Wizara ya Mambo ya Nje, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian katika ujumbe aliotuma kwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiislamu, ameitaja sikukuu ya Idul Fitr kuwa sherehe ya kushukuru baada ya mwezi wa ibada na kumcha Mwenyezi Mungu. Aidha ameitaja sherehe ya Idul Fitr kuwa wakati wa urafiki, udugu na umoja wa Waislamu kwa ajili ya kufikia malengo matukufu ya Uislamu.

Katika ujumbe wake kwa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi za Kiislamu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia ushirikiano wa viongozi wa nchi za Kiislamu katika kuimarisha mshikamano wa Waislamu na maendeleo ya jamii za Kiislamu.