Iran na Iraq zasisitiza umuhimu wa kupanua zaidi ushirikiano baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i96588-iran_na_iraq_zasisitiza_umuhimu_wa_kupanua_zaidi_ushirikiano_baina_yao
Mataifa jirani ya Iran na Iraq yamesisitiza azma yaliyonayo ya kupanua na kustawisha zaidi ushirikiano baina yao katika nyanja mbalimbali.
(last modified 2026-07-11T07:59:36+00:00 )
Apr 23, 2023 07:48 UTC
  • Iran na Iraq zasisitiza umuhimu wa kupanua zaidi ushirikiano baina yao

Mataifa jirani ya Iran na Iraq yamesisitiza azma yaliyonayo ya kupanua na kustawisha zaidi ushirikiano baina yao katika nyanja mbalimbali.

Sisitizo hilo limebainishwa katika mazungumzo ya njia ya simu baina ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Muhammad Shia' al-Sudan Waziri Mkuu wa Iraq ambapo wamepeana mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Eidul-Fitr.

Viongozi hao sambamba na kubadilishana mawazo kuhusiana na uhusiano wa pande pande, matukio ya kieneo na kimataifa wamesisitiza azma ya serikali zao ya kuwa na uhusiano wenye wigo mpana zaidi.

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mazungumzo yake hayo na Waziri Mkuu wa Iraq juu ya udharura wa kutekelezwa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande mbili.

Muhammad Shia' al-Sudan Waziri Mkuu wa Iraq katika moja ya safari zake mjini Tehran akizungumza na Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya kiislamu 

Amebainisha kuwa, kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano hayo kutaandaa uwanja wa kuimarishwa zaidi kiwango cha ushirikiano baina ya mataifa haya mawili jirani yenye uhusiano mkongwe.

Kwa upande wake, Mohammed Shia' Al-Sudani Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza udharura wa kuinuliwa kiwango cha ushirikiano baina ya Tehran na Baghdad kadiri inavyowezekana hasa kwa kuzingatia uwezo wa mataifa haya, kuwa na ukuuruba pamoja na mashirikiano ya kiutamaduni na kihistoria.

Iran na Iraq zimewekewa vikwazo mara chungu nzima na madola ya Magharibi na kila mara ziliposhirikiana ziliweza kuvuka kirahisi vizingiti na vikwazo hivyo vya kiuchumi dhidi yao.