Iran: Vita si njia ya kuutatua mgogoro wa Ukraine
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa kimsingi wa Tehran kuhusiana na mgogoro wa Ukraine na kusisitiza kwamba, vita kamwe haviwezi kuwa njia sahihi ya kutatua kadhia hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo na Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura na kujadiliana naye masuala mbalimbali muhimu ya kibinadamu kama ya Syria, Yemen, Afghanistan na Ukraine na kusema kuwa, msimamo wa Iran kuhusu kadhia ya Ukraine uko wazi na daima Tehran inasisitiza kuwa, vita haviwezi kutatua mgogoro huo na haiusaidii kijeshi upande wowote ule kwenye mgogoro huo.
Vile vile amesema, msimamo wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuheshimu haki ya kujitawala nchi zote duniani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia jinsi Iran ilivyowapokea na kuwapa hifadhi mamilioni kadhaa ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Afghanistan na ameutaka Umoja wa Mataifa uisaidie Tehran katika kutatua changamoto za wakimbizi hao.
Kwa upande wake, Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura ametumia mazungumzo yake hayo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, kutoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya kibinadamu huko Afghanistan na Ukraine.