Raisi: Wazayuni hawawezi kujidhaminia usalama wao
Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Iran amesema: Hali ya mambo hivi sasa imebadilika na kwamba utawala wa Kizayuni hauwezi kujidhaminia usalama ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.
Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya al Mayadeen, Rais Sayyid Ebrahim Raisi ameashiria matatizo ya ndani yanayouzonga utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa:Mikataba kama ule wa Sharam- Sheikh, wa Oslo na Camp David haiwezi kuudhaminia utawala huo usalama. Amesema,leo hii uamuzi uko mikononi mwa mujahidina wa Kipalestina na si katika meza ya mazungumzo ya kisiasa.
Rais wa Iran amegusia pia kuhusu uwezo wa kijeshi na kiulinzi wa nchi hii na kusema: Katika upande wa uwezo wa kijeshi na kiulinzi si tu Iran imeweza kujitegemea bali ni kati ya nchi zilizopiga hatua katika sekta ya ulinzi duniani. Raisi amesisitiza kuwa: Katika miaka 44 iliyopita adui hajafanya uinga wowote dhidi ya Iran si kwa sababu hakutaka bali ni sababu hana ubavu wa kufanya hivyo.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Rais Ebrahim Raisi ameashiria kujiunga Iran na Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai na kueleza kuwa: Hatua hiyo imeisaidia Iran kuandaa mazingira ya kushirikiana na miundomsingi ya Asia na pia tuko tayari kujiunga na kundi la BRICS.
Kuhusu uhusiano wa Iran na Saudi Arabia, Rais wa Iran ameongeza kuwa: Iran na Saudi Arabia ni nchi mbili zenye taathira katika eneo la Mashariki ya Kati na uhusiano wa pande mbili utakuwa na manufaa mengi. Wakati huo huo amezungumzia kukasirishwa utawala wa Kizayuni na kuhuishwa uhusiano kati ya Iran na Saudia na akasema: Maadui khususan utawala wa Tel Aviv wamekasirishwa na hatua hii na sababu yake ni njama wanazofanya za kueneza migawanyiko.