May 31, 2023 05:50 UTC
  • Nafasi ya BRICS duniani na umuhimu wake kwa Iran

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atasafiri hivi karibuni kuelekea Cape Town, Afrika Kusini, kwa ajili ya kushiriki katika mkutano ujao wa BRICS .

Mehdi Safari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia diplomasia ya uchumi katika Wizara ya Masuala ya Kigeni ya Iran amesema kuhusu mchakato wa uanachama wa Iran katika jumuiya ya  BRICS kwamba nchi wanachama wa BRICS bado hazijaainisha vigezo vyao kwa ajili ya kuwapokea wanachama wapya, lakini kwa kuzingatia vigezo ilivyonavyo Iran, inaweza kufungamana kirahisi na vigezo vyo vyote vya kundi hilo.

BRICS ni jina la kundi linaloongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi, ambalo linaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Nchi hizo zitakutana mjini Cape Town Juni 2 hadi 3 kujadili njia za kupanua kundi hilo. Iran, Saudi Arabia, Argentina, Umoja wa Falme za Kiarabu, Algeria, Misri, Bahrain na Indonesia zimetangaza nia yao ya kutaka kujiunga na BRICS.

Kufuatia kuingia madarakani serikali ya 13 inayoongozwa na Rais Ebrahim Raisi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeimarisha siasa za kuboresha uhusiano wa kisiasa na kibiashara na nchi jirani pamoja na waitifaki wake katika eneo la Mashariki, siasa zinazolenga kuufungua uchumi wa Iran na kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi vya Marekani. Kwa hakika katika kipindi hiki siasa za nje za Iran zimejikita katika kustawisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa wa pande kadhaa na nchi hizo kwa kujaribu kuwa mwanachama wa asasi za kieneo na kimataifa kama vile Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Hossein Amir-Abdollahian

Hivyo juhudi za Iran kwa ajili ya kujiunga na BRICS zinaweza kutathminiwa kuwa ni katika hatua zake za diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuimarisha uhusiano wake na nchi za eneo na kimataifa. Moja ya sababu muhimu zaidi za umuhimu wa kundi la BRICS ambalo lina uwezo mkubwa wa kiuchumi duniani, ni ukuaji wa kasi wa uchumi na ushawishi wake katika masuala ya kimataifa na bila shaka unatokana na kuwa na nusu ya watu wote duniani, linaunda asilimia 25 hadi 28 ya uwezo wa kiuchumi duniani na lina utajiri mkubwa wa nguvukazi na maliasili.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndipo Marekani ikawa mmoja wa wapinzani wakubwa wa kustawi kundi la BRICS na imekuwa ikitumia kila mbinu kuwashawishi washirika wake wa Magharibi wazuie kuimarika kwake katika ngazi za kimatifa. Mchakato wa maendeleo ya kiuchumi na kiviwanda wa wanachama wa BRICS unaonyesha kuwa harakati na fikra za kundi hilo linaloinukia kiuchumi zimejengeka katika msingi wa kuwa na nafasi muhimu katika ulimwengu ujao wa kambi kadhaa zenye nguvu, jambo linalochukuliwa na mfumo unaotawala sasa duniani kuwa tishio kubwa kwa sualama wake.

Masuala ya kiuchumi kama vile mifumo ya benki, nishati, usafiri, mawasiliano ya simu, masuala ya kijamii na kazi ni mambo muhimu zaidi ya kiuchumi yanayozingatiwa na kundi hili. Lengo jingine la BRICS ni kujitenga na dola kama sarafu ya kawaida ya biashara ya kimataifa, na sasa suala la kuanzisha "hazina ya kimataifa ya sarafu" kwa kuzingatia sarafu za nchi wanachama linaendelea kujadiliwa. BRICS pia anajaribu kukabiliana na taasisi za fedha za Magharibi kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa kwa kuunda benki mpya ya maendeleo na hifadhi ya sarafu ya pamoja. Kila moja ya nchi wanachama wa kundi la BRICS inachukuliwa kuwa mhusika mkuu katika nyanja za kisiasa au kiuchumi katika maeneo yao. Nafasi ya kipekee ya kijiografia ya Iran na uwezo wake katika nyanja za nishati, usafiri na biashara umewafanya wanachama wa BRICS kutoa kipaumbele maalumu kwa Iran kama njia ya dhahabu ya kuunganisha maeneo ya Mashariki na Magharibi ya dunia.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Shanghai

Kwa hiyo, uanachama wa Iran kama mmoja wa wadhamini wakubwa wa nishati na wenye uwezo mkubwa wa kupitishia bidhaa za nchi wanachama unaweza kuwa na nafasi muhimu kwa BRICS kwa sababu inatoa fursa nyingi za kiuchumi kwa wanachama wa kundi hilo. Ikumbukwe pia kwamba Iran inahitajia uwekezaji wa kiuchumi wa kigeni ili kuboresha uchumi wake, kwa hivyo, kuwepo vitega uchumi vya wanachama wa BRICS kunaweza kuchukuliwa kuwa fursa nzuri kwa Iran. Katika upande wa siasa vile vile, ushirikiano na uanachama wa Iran katika BRICS ni muhimu sana. Kwa kutilia maanani kuwa kundi la BRICS limeundwa bila uanachama wa nchi za Ulaya na Marekani, na kwa kutilia maanani vikwazo vya upande mmoja na mashinikizo ya kisiasa ya Marekani na Ulaya dhidi ya Iran, uanachama wa Tehran katika kundi hilo unaweza kuchangia pakubwa katika kupunguza makali ya vikwazo na siasa za mashinikizo za nchi za Magharibi dhidi yake, hasa kwa kuzingatia uwezo mkubwa wa kiuchumi na kisiasa wa nchi kama vile China, Russia na katika kundi hilo.