Jun 07, 2023 01:23 UTC
  • Kombora la Hypersonic la Fattah; matunda ya kimapinduzi na uainishaji hatima katika vita vya kisasa

Jumanane ya jana tarehe 6 Juni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua kombora lake la kwanza la balistiki la Hypersonic lililopewa jina la 'Fattah'.

Rais Ebrahim Raisi, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH), Meja Jenerali Hossein Salami, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la SEPAH, maafisa wa ngazi za juu serikalini na makamanda wa vikosi vya ulinzi vya Iran walishiriki katika hafla ya uzinduzi wa kombora hilo uliofanyika katika moja ya kambi za Kikosi cha Anga cha Jeshi la SEPAH.  Makombora ya Hypersonic yana kasi mara tano zaidi ya mwendo wa sauti, na hivyo kuyapa uwezo wa aina yake wa kutoweza kuyatungua.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Ibrahim Raisi wa Jamhurii ya Kiislamuu ya Iran sambamba na kusisitiza kwamba, sekta ya ulinzi na makombora ya Iran inategemea wataalamu wa ndani alisema: Nguvu na uwezo wa Iran wa kumfanya adui asishambulie ni nukta ya usalama na amani ya kudumu kwa mataifa ya eneo.

Kabla ya hapo, Brigedia Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapiinduzi ya Kiislamu SEPAH alisema, kombora hilo jipya la balestiki la Hypersonic lililoundwa kikamilifu na wataalamu wa Iran, mbali na kuwa na uwezo wa kupenya kwenye mifumo ya kisasa ya kutungua makombora, lakini lina uwezo mkubwa wa kupiga shabaha kwa usahihi mkubwa. Kadhalika, kombora hilo la Hypersonic lililopewa jina la 'Fattah' lina kasi kubwa na uwezo wa aina yake, na hakuna teknolojia yoyote duniani inayoweza kulitungua hata katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo, kama ambavyo, lina uwezo wa kupiga umbali wa kilomita 1,400, sambamba na kutambua na kuharibu ngao za aina zote za makombora.

Makombora ya Hypersonic ni katika silaha za kisasa zaidi ambazo leo hiii zinazalishwa na mataifa kama Russia, China na Marekani. Kwa muktadha huo, kutokana na utaalamu wa hali juu unaohitajika kwa ajili ya kutengeneza makombora haya, ni mataifa machache mno duniani ambayo yana uwezo wa kubuni, kutengeneza na kuzalisha makombora ya aina hii.

Kufanikiwa Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran kufikia teknolojia hii ya kutengeneza makombora ya kisasa zaidi ya Hypersonic hapana shaka kuwa hili ni tukio la kimapinduzi na lenye kuainisha hatima katika uga wa vita vya kisasa. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana kuanzia sasa na kuendelea, maadui wa Iran ya Kiislamu hususan utawala wa Kizayuni wa Israel hawatakuwa na budi isipokuwa kuangalia upya na kwa makini mahesabu yao katika uga wa vitisho vya kutaka kuishambulia kijeshi Iran.

Israel ambayo hadi kufikia sasa daima imekuwa ikidai kuwa na uwezo wa kukabiliana na mashambulio ya balestiki ya Iran sasa haina budi isipokuwa kukiri kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na kombora la kisasa la Hypersonic la Fattah, kombora ambalo lina uwezo wa kutumia sekundu 400 tu mpaka kufika Israel. Kimsingi makombora ya Hypersonic ni silaha muhimu sana kutokana na kuwa, mpaka sasa hakuna mbinu ya kutegemea ya kuliona likipenya na kuweza kuliangamiza. Madola ya Magharibi hayana uwezo wa kukabiliiana na makombora ya Hypersonic na mfumo wa makombora wa Magharibi umeshindwa kukabiliana na makombora hayo tangu Russia ilipoyatumia katika vita vya Ukraine.

Mintarafu hiiyo inapasa kusema kuwa, kuzinduliwa kombora la Hypersonic la Fattah la Iran ni kufunguliwa ukurasa mpya katika uga wa utengenezaji silaha ambao una uwezo wa kubadilisha hatima ya vita, chambilecho Waingereza hilo litakuwa ni "game change weapon." Hapana shaka kuwa, uzinduzi wa kombora la Hypersonic la Fattah la Iran ni tukio jipya katika eneo la Asia Magharibi ambalo ni kwa maslahi ya Iran na litawalazimisha maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutazama upya mahesabu yao kuhusiana na kila hatua ya chuki na uadui wanayotaka kuichukua dhidi ya Iran.

Tags