Iran yasema Marekani ni mshirika wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel wa kumuua mtoto mchanga wa Kipalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kusema Marekani pia ni mshirika katika jinai za kila siku za Israel kutokana na uungaji mkono wake wa mara kwa mara kwa utawala huo unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina.
Nasser Kan'ani aliyasema hayo katika chapisho kwenye akaunti yake ya Twitter siku ya Jumanne, siku moja baada ya Mohammad Haytham Tamimi aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu kufariki dunia kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata siku chache zilizopita kutokana na kupigwa risasi na wanajeshi katili wa Israel.
“Mohammad Haytham Tamimi, mtoto wa miaka miwili, ni mtoto wa 28 wa Kipalestina asiye na hatia ambaye ameuawa mikononi mwa utawala wa Israel unaoua watoto. Waungaji mkono na wafadhili wa utawala huu katika uhalifu huu wa kila siku pia wanabeba lawama za jinai hizo kwa mtazamo wa kisheria na kimataifa,” aliandika.
Mohammad alipigwa risasi kichwani katika kijiji cha Nabi Salah, karibu na Ramallah, na wanajeshi wa Israel siku ya Alhamisi, wakati yeye na baba yake, Haytam Tamimi, walipokuwa kwenye gari lao lililoegeshwa nje ya nyumba yao.
Alipata majeraha mabaya kichwani huku babake akipata majeraha kifuani. Walipelekwa hospitalini, ambapo mtoto huyo wa Kipalestina alifariki Jumatatu asubuhi.
Kan'ani pia alibainisha kuwa sadfa ya jinai hiyo ya kutisha na maoni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken katika Kamati ya Masuala ya Umma ya Israel ya Marekani (AIPAC) kuhusu misaada na uungaji mkono wa kila mwaka wa Marekani kwa utawala wa Israel ni sawa na Washington. kushiriki katika uhalifu wa kila siku wa utawala huo ghasibu.
Vikosi vya Israel huvamia miji mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu karibu kila siku kwa kisingizio cha kuwaweka kizuizini Wapalestina wanaopigania ukombozi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Middle East Eye, wanajeshi wa Israel na walowezi wa Kizayuni wameua Wapalestina wasiopungua 119 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds (Jerusalem) Mashariki tangu Januari na wengine 34 katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.
Aidha jumla ya watoto 28 wameuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel tangu mwanzoni mwa mwaka huu, wakiwemo saba katika Ukanda wa Gaza.