"Kupanuka muqawama, chachu ya kuporomoka Israel"
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kuendelea kuenea harakati za muqawama katika maeneo yote ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu ni chachu ya kusambaratika na kuporomoka kwa kasi utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ali Akbar Ahmadian amesema hayo katika mazungumzo yake na Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, "Kupanuka kambi ya muqawama huko Palestina, si tu kutavuruga njozi za Israel, lakini kutakuwa chachu ya kuporomoka kwa utawala huo ghasibu."
Ahmadian amesema ushindi wa karibuni wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina katika vita vya siku 5 dhidi ya hujuma ya kinyama ya utawala huo unathibitisha wazi ukweli huo wa kusambaratika Wazayuni.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amepongeza kitendo cha kusimama kidete na kupambana kishujaa wanamuqawama wa Palestina, hasa Harakati ya Jihad Islami katika vita hivyo vya mwezi Mei mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge la Iran katika mazungumzo yake na Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema umoja wa umma wa Kiislamu umepelekea kambi ya muqawama kuwa na nguvu na kuimarika zaidi.
Mohammad Baqer Qalibaf amesema Palestina ndiyo kadhia kuu ya ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa, na kusisitiza pia kwamba Palestina ndiyo mbeba bendera ya mrengo wa muqawama.
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina kwa upande wake, ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake wa daima kwa wananchi wa Palestina na mapambano yao na amewasilisha ripoti kuhusu matukio ya hivi karibuni huko Palestina na kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 5 ulivyovianzisha dhidi ya Gaza mwezi uliopita wa Mei.