Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kisayansi kati ya Iran na Uzbekistan ni wa kipekee
(last modified Mon, 19 Jun 2023 04:41:02 GMT )
Jun 19, 2023 04:41 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kisayansi kati ya Iran na Uzbekistan ni wa kipekee

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza jana katika mazungumzo na Rais wa Uzbekistan hapa Tehran kwamba uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kisayansi kati ya Iran na Uzbekistan ni wa kipekee.

Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana Jumapili alikutana na kuzungumza na Rais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan na ujumbe aliofuatana nao ziarani hapa nchini. Katika mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi aliashiria  uhusiano wa aina yake ya kihistoria, kiutamaduni na kisayansi kati ya nchi mbili za Iran na Uzbekistan na kusema: Maeneo haya ya pamoja yanapasa kutumiwa kwa ajili ya kupanua mahusiano katika nyanja mbalimbali. 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameeleza kufurahishwa na kuridhishwa kwake na  kuhuishwa uhusiano baina ya nchi mbili hizi baada ya kupita kipindi kirefu na kuongeza kuwa: Kwa miaka mingi uhusiano kati ya Iran na Uzbekistan ulikuwa wa kiwango cha chini na tunataraji kuwa ziara hii na mazungumzo yaliyofanyika hapa Tehran yatakuwa mwanzo wa mustakbali mwema katika uhusiano wa nchi mbili.  

Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo wa kuiunganisha kwa urahisi Uzbekistan na maji huru kupitia Turkmenistan na Afghanistan; huku nyanja za ushirikiano zikiwa zaidi ya biashara na usafirishaji na hilo linaweza kufikiwa pakubwa kupitia ubunifu mbalimbali katika sekta za sayansi na teknolojia na nyanja nyinginezo.

Ujumbe wa Uzbkestan ukiwa kwenye mazungumzo na wa Iran mjini Tehran

Ameiongeza kuwa: Bila shaka kupanuliwa uhusiano wa Iran na Uzbkekistan una wapinzani wake lakini uamuzi unapasa kuchukuliwa bila kuzingatia upinzani ulioko, na wakati huo huo ushirikiano unapasa kupanuliwa kadiri inavyowezekana kwa mujibu wa maslahi ya nchi mbili. 

Katika mazungumzo hayo ya jana hapa Tehran ambayo yalihudhuriwa pia na Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais  Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan ameyataja mazungumzo yake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa  ya kihistoria na kusema: Tulisikitishwa na hali iliyokuwepo ya kusita kwa uhusiano kati ya nchi  mbili na kupungua kwa ushirikiano, na tunaraji kwamba kufuatia mazungumzo yaliyofanyika Tehran hatua kubwa zitachukuliwa na ushirikiano wa pande mbili katika nyanya za kibiashara, usafirishaji, sayansi, teknolojia na utalii utafika katika kiwango killichokusudiwa.   

Katika mazungumzo hayo Rais wa Uzbekistan amepongeza msimamo imara wa taifa la Iran mkabala wa vikwazo na kuongeza kuwa, mafanikio ya Iran khususan katika sekta za sayansi na teknolojia ambayo baadhi yake tumeyashuhudia katika maonyesho yaliyofanyika yanaonyesha kuwa nchi inaweza kufikia na kutimiza lengo lake kuu kutokana na uongozi wa busara wa kiongozi wake na  umoja licha ya mashinikizo yote dhidi yake.