Iran: Madola ya Kiislamu yachukue hatua za kukomesha jinai za Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyaasa madola ya Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake na Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Iran itaendelea kuunga mkono kadhia ya Palestina na Quds Tukufu, kama ambavyo itayasaidia mapambano ya makundi halali ya muqawama ya Wapalestina mkabala wa Israel.
Amir-Abdollahian amesema utawala wa Kizayuni ndio mzizi wa ukosefu wa usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi na kusisitiza kuwa, umoja wa umma wa Kiislamu tu ndio unaoweza kuzima jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wanaodhulumiwa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, kushirikiana serikali na mataifa ya Kiislamu kutakuwa na mchango mkubwa katika kulinda na kuhami matukufu ya Kiislamu katika mji mtakatifu wa Quds.
Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amepongeza ushindi wa karibuni wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina katika vita vya siku 5 dhidi ya hujuma ya kinyama ya utawala huo katika Ukanda wa Gaza.
Kwa upande wake, Ziad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake wa daima kwa wananchi wa Palestina na kambi ya muqawama.
Ameeleza bayana kuwa, makundi ya muqawama hivi sasa yapo imara na katika hali nzuri, na ndiposa yanapata ushindi mtawalia dhidi ya utawala pandikizi wa Israel.