Jun 24, 2023 10:07 UTC
  • Iran yalaani hatua ya Wazayuni wa Israel ya kuchoma moto Qur'ani Tukufu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali kitendo cha walowezi wa Kizayuni cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu wakati wa mashambulizi ya askari wa Israel dhidi ya misikiti katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe wa Twitter na kueleza kuwa, "Wazayuni kuvamia misikiti, kuvunjia heshima Qurani Tukufu, kuvunja nyumba za Wapalestina, na kuua watoto, wanawake na watu wasio na ulinzi wa Palestina kila uchao, ni ishara kuwa utawala wa Kizayuni hauheshimu mistari yoyote myekundu."

Kan'ani ameeleza bayana kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hauna mipaka katika mienendo yake ya uvamizi, kukanyaga haki za binadamu na kuvunjia heshima matukufu ya kidini.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, utawala haramu wa Israel umepata uthubutu wa kuendeleza jinai na ukatili wake dhidi ya Wapalestina, kutokana na kimya cha jamii ya kimataifa, na vilevile himaya na kupewa msaada na uungaji mkono na Wamagharibi. 

Uafriti wa Wazayuni wa kunjia heshima Qurani Tukufu mjini Al-Khalil

Walowezi wa Kizayuni Alkhamisi usiku walivamia Msikiti wa al-Ribat katika kitongoji cha Urif kusini mwa mji wa Nablus, na kuchoma moto nakala za Qurani Tukufu. Video ya kamera ya CCTV imeonyesha Wazayuni hao waliokuwa wamefunika nyuso zao wakichana na kuchoma moto nakala za Qurani Tukufu ndani ya msikiti huo.

Walowezi hao wa Kizayuni hawakuishia hapo, bali walienda mbali zaidi na kuingiza mbwa ndani ya msikiti huo. Vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu vimeumiza hisia za Waislamu kote dunia.

Tags