Rais wa Iran aalikwa kuhudhuria mkutano wa BRICS Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i99516-rais_wa_iran_aalikwa_kuhudhuria_mkutano_wa_brics_afrika_kusini
Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amealikwa rasmi kuhudhuria mkutano ujao wa kundi la BRICS utakaofanyika nchini Afrika Kusini.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 04, 2023 03:54 UTC
  • Rais wa Iran aalikwa kuhudhuria mkutano wa BRICS Afrika Kusini

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amealikwa rasmi kuhudhuria mkutano ujao wa kundi la BRICS utakaofanyika nchini Afrika Kusini.

Katika mazungumzo yake ya simu na Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran jana Jumatatu, Naledi Pandor, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini alisema Rais Cyril Matamela Ramaphosa wa nchi hiyo ametuma mwaliko rasmi wa kumuomba Rais wa Iran ashiriki katika mkutano ujao wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa kundi la BRICS utakaofanyika mjini Johannesburg, kuanzia Agosti 22 hadi 24 mwaka huu 2023.

Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran ipo tayari kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili wa nchi hii na Afrika Kusini katika nyuga tofauti hasa za uchumi na biashara.

Kadhalika amepongeza hatua ya Iran na Afrika Kusini kuafikiana tarehe ya kufanyika mkutano wa Kamisheni ya Pamoja ya Uchumi, akisisitiza kuwa Tehran ipo tayari kuwa mwenyeji wa kikao hicho.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Afrika Kusini

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema Iran inaweza kuwa mshirika endelevu wa kuunganisha nchi wanachama wa BRICS katika maeneo muhimu ya kupitisha nishati na masoko makubwa duniani kwa kuzingatia nafasi yake ya kipekee ya jiografia ya kisiasa na jiografia ya kiuchumi.

Kwa mujibu wa Sayyid Raisi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetimiza vigezo vyote vya kukubaliwa kuwa mwanachama wa kundi hilo la BRICS.

Aidha Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran karibuni alienda Cape Town nchini Afrika Kusini, kwa ajili ya kushiriki mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa kundi la BRICS.