Iran yajitosheleza kikamilifu katika sekta ya uchimbaji mafuta na gesi
Waziri wa Mafuta wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu sasa inajitosheleza kikamilifu katika sekta ya uchimbaji mafuta na gesi, baharini na katika nchi kavu.
Mhandisi Javad Owji amesema hayo pambizoni mwa semina ya kimataifa ya wazalishaji wakuu wa mafuta duniani OPEC mjini Vienna, Austria na kumwambia mwandishi wa shirika la habari la Iran Press kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa kama hayo licha ya kuwa chini ya mashinikizo ya makumi ya miaka.
Amesema, mchakato wote wa uchimbaji na utafutaji mafuta na gesi kuanzia sifuri hadi asilimia mia moja unafanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe iwe ni katika maeneo ya majini au ya nchi kavu.
Waziri Owji ameongeza kuwa, wataalamu wa Iran wameweza kikamilifu, kuziba pengo la vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi katika sekta ya mafuta na gesi humu nchini.
Amesema, hivi sasa Iran inajitosheleza kikamilifu katika sekta zote zinazohusiana na mafuta na gesi na haihitajii chochote kutoka nje ya nchi katika kazi zake hizo.
Waziri wa Mafuta wa Iran vile vile amesema kuhusu akiba ya rasilimali hiyo muhimu humu nchini kwamba, unapojumuisha kila kitu utaona kuwa Iran inashika nafasi ya kwanza ya kuwa na akiba kubwa zaidi ya mafuta na gesi duniani.
Semina wa nane ya kimataifa ya OPEC ilifanyika Vienna, Australia jana Jumatano na kuhudhuriwa na wazalishaji wakuu wa mafuta na gesi pamoja na watumiaji wa nishati hizo muhimu. Miongoni mwa ajenda kuu za semina hiyo ilikuwa ni kuzingatiwa usalama wa mazingira katika utumiaji wa nishati hizo.