Jul 25, 2023 11:44 UTC
  • Imarati na Qatar katika mkondo wa kupanua mahusiano

Amir wa Qatar amemteua Sultan Salmeen Saeed Al-Mansouri kuwa balozi wa mpya wa nchi hiyo katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mwezi Juni 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilitangaza kukata uhusiano wao wote na Qatar na kuiwekea vikwazo vya kila upande vya angani, baharini na ardhini nchi hiyo. Raia na wanadiplomasia wa Qatar waliokuweko kwenye nchi hizo nne za Kiarabu walitimuliwa kijeuri na hilo likakuza mgogoro mkubwa katika Ulimwengu wa Kiarabu. Nchi hizo zilidai kuwa zimechukua hatua hiyo dhidi ya Qatar kwa kile walichokiita kuunga mkono ugaidi na kuvuruga utulivu wa eneo hilo, madai ambayo Qatar iliyakanusha vikali.

Katika kipindi cha miaka mitatu na nusu, mataifa hayo manne yaliishinikiza vikali Qatar ili kuifanya nchi hiyo isalimu amri na kukubali matakwa yao. Hata hivyo Qatar ikiungwa mkono na kusaidiwa na Uturuki na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweza kusambaratisha mashinikizo ya kila upande ya mataifa hayo.

Baada ya Donald Trump kubwagwa katika awamu ya pili ya uchgauzi wa Rais nchini Marekani, kulianza kuonekana mabadiliko katika sera za kigeni za Saudi Arabia.

Baada ya kuona mashinikizo na vikwazo vyao vimeshindwa kuipigisha magoti Qatar, mwaka 2021, Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zilitangaza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Doha. Zilitangaza hayo pambizoni mwa Mkutano wa 41 wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi uliofanyika Al-Ula, Saudi Arabia Januari 2020. Baada ya kuhuishwa uhusiano baina ya Riyadh na Doha, mataifa mengine matatu ya Imarati, Bahrain na Misri nayo yalipiga hatua moja mbele kwa shabaha ya kuhuisha uhusiano na Doha.

 

Hivi sasa Sultan Salmeen Saeed Al-Mansouri ameteuliwa kuwa balozi wa kwanza wa Qatar baada ya Doha na Abu Dhabi kuhuisha uhusiano katika hali ambayo, tarehe 19 ya mwezi huu wa Julai mataifa hayo mawili yalitangaza kurejesha kikamilifu uhusiano wao wa kidiplomasia baina yao ambapo ubalozi wa Qatar huko Abu Dhabi na ubalozi wake mdogo wa mjini Dubai, pamoja na ubalozi wa Imarati mjini Doha zilianza tena kazi rasmi wiki iliyopita. Katika taarifa yao ya pamoja nchi hizo zilitangaza kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa makubaliano ya al-Ula na shauku na hamu ya nchi mbili hizo ya kuimarisha na kustawisha uhusiano wao.

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita pia, uhusiano wa Imarati na Qatar umechukua mkondo wa kuongezeka kwani viongozi wa nchi hizo wakiwa na lengo la kuongeza kiwango cha ushirikiano kwa mujibu wa matokeo ya mkutano wa al-Ula wa Saudia, wamefanya mikutano na mazungumzo mengi. Amir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Aal-Thani mwezi Mei mwaka jana (2022) kwa mara ya kwanza alifanya safari nchini Imarat baada ya kupita miaka mitano. Aidha Muhammad bin Zayd al-Nahyan, Rais wa Imarati Disemba 5 mwaka uliopita naye alifanya safari ya kwanza tangu kuibuka mgogoro wa mataifa hayo ya Ghuba ya Uajemi na hatua yao ya kukata uhusiano wa kidiplomasia na Qatar mwaka 2017.

 

Filihali, balozi wa Qatar anaelekea Abu Dhabi kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 6 katika hali ambayo, kumetokea mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sera za kigeni za mataifa ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi. Baada ya mfalme Salman bin Abdul Aziz kushika hatamu za uongozi wa Saudia 2015 na kuchukua madaraka na mamlaka hatua kwa hatua Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, walimwengu walishuhudia sera za kigeni za Riyadh zenye mizozo na mivutano.

Hata hivyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita hali ya mambo imebadilika kikamilifu ambapo Riyadh imechukua mkondo wa sera za mazungumzo, mapatano na maridhiano, ambapo Machi mwaka huu kulishuhudiwa kufikiwa makubaliano ya kuhuishwa uhusiano baina yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  Katika upande mwingine Qatar na Imarati zinafuatilia suala la kupanua ushirikiano na uhusiano baina yao katika hali ambayo, hivi karibuni duru za habari ziliripoti juu ya kuibuka hitilafu kubwa katika uhusiano wa Saudi Arabia na Imarati.

Tags