Vita vya maneno baina ya Taliban na serikali ya Pakistan vingali vinaendelea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amelihutubu kundi la Taliban linalotawala nchini Afghanistan akisema: "amani na usalama wa Pakistan haviwezi kufanyiwa mchezo".
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Bilawal Bhutto Zardari, amesisitiza ulazima wa kuwa na maelewano na Kabul sambamba na kueleza bayana kuwa amani na usalama wa Pakistan haviwezi kufanyiwa mchezo.
Zardari, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Watu wa Pakistan amebainisha pia hamu ya nchi yake ya kuwa na maelewano ya dhati na ya ujengaji, kikanda na kimataifa kwa lengo la kuimarisha amani, usalama na utulivu nchini Afghanistan.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid, alikanusha tuhuma zilizotolewa na Islamabad dhidi ya serikali ya kundi hilo. Sambamba na kupinga ufanyaji mashambulizi ya kigaidi ndani ya Pakistan, Mujahid alirudia na kutilia mkazo ahadi ya kundi hilo kwa kusema, "serikali ya mpito ya Taliban haitaruhusu mtu au kikundi chochote kutumia ardhi ya Afghanistan dhidi ya Pakistan, lakini Kabul haina masuulia ya kuzuia mashambulizi yanayofanywa ndani ya ardhi ya Pakistan na badala ya kuzusha tuhuma, viongozi wa Pakistan inawapasa wafanye juhudi za kuimarisha usalama wa nchi hiyo".
Hadi kitambo si kirefu nyuma, Pakistan ilikuwa ikijulikana kama muungaji mkono wa Taliban. Lakini katika miezi ya karibuni, uhusiano kati ya nchi hiyo na Afghanistan iliyo chini ya utawala wa Taliban umetawaliwa na mikwaruzano na mivutano.