Mar 16, 2024 02:22 UTC
  • Ombi la jamii ya Shia wa Afghanistan kwa kundi la Taliban

Wawakilishi wa jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan wamewasilisha mapendekezo yao ya maandishi kwa Mohammed Abdul Kabir, naibu wa masuala ya kisiasa wa Waziri Mkuu wa utawala wa Taliban.

Mapendekezo hayo yamewasilishwa kufuatia hatua ya Taliban ya kutozingatia matakwa ya jamii ya Waislamu wa madhehebu ya  Shia nchini Afghanistan. 

Hii si mara ya kwanza kwa wanazuoni wa jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Afghanistan kuwasilisha maombi yao kwa mamlaka ya Taliban, ana kwa ana na kwa njia ya maandishi. Inatupasa kusema kuwa, licha ya maafisa wa Taliban kukubali kwa maneno kwamba wamekubali mapendekezo ya jamii hiyo, lakini hadi sasa hawajachukua hatua yoyote ya kivitendo ya kutimiza haki za Waislamu wa madhehebu hiyo. Mara hii pia maafisa wa utawala wa Taliban wameahidi kuwa watachunguza mapendekezo ya jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan. 

Miongoni mwa matakwa ya Mashia wa Afghanistan ni kutambuliwa rasmi madhehebu ya Ja'fari katika utawala wa Taliban, kufundishwa fiqhi ya madhehebu ya Ja'fari katika vyuo vikuu na shule kwa wanafunzi wa Kishia na kushirikishwa ipasavyo Waislamu wa madhehebu ya Shia katika ofisi za serikali na masuala ya kiidara.

Asadollah Bashir, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Jamii ya Waislamu wa Kishia ya Afghanistan daima imekuwa ikishirikiana vyema na Taliban katika nyanja ya utawala, na wanaamini kwamba ushirikiano wa wafusi wa madhehebu zote za Kiislamu nchini Afghanistan, utaiwezesha Taliban kuwa na utawala wenye mafanikio. Hii ni kwa sababu, nchi hii ina jamii ya watu wa kabila, mbari na madhehebu tofauti, na hapana shaka kwamba suala la kuimarisha amani na utulivu linahitaji ushirikiano wa kitaifa kati ya mirengo yote ya kisiasa, kimadhehebu na kikabila."

Wanazuoni wa Shia, Afghanistan

Ijapokuwa Taliban imetangaza madhehebu yake rasmi kuwa ni ya Hanafi, lakini inasisitiza suala la kuheshimiwa haki na sheria za kifiqhi za madhehebu nyingine hasa za Waislamu wa madhehebu ya Mashia; lakini inasikitisha kuwa kiutendaji, Taliban haionyeshi nia ya dhati ya kutekeleza suala hilo. Haya yote ni licha ya kwamba, jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya Afghanistan daima imekuwa ikishirikiana vyema na utawala wa Taliban katika kipindi cha miaka miwili iliyopita tangu kundi hilo iliporejea madarakani. Kundi hilo bado linazuia utekelezaji wa sheria za mtu binafsi za fiqhi ya Ahlul Bayt na pia ufundishaji wa sheria hizo katika vyuo vikuu na shule za Mashia za Aghanistan.

Ikumbukwe kuwa baada ya Hanafi, ambayo Taliban imetangaza kuwa ndiyo madhehebu rasmi ya Afghanistan, Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaunda jamii kubwa zaidi ya kidini nchini Afghanistan. Kwa msingi huo, inatazamiwa kuwa watawala w a Taliban wataheshimu haki zao za kiraia na kidini na kuwaruhusu kutenda na kutekeleza ibada zao kwa mujibu wa sheria zao za kifiqhi. 

Waislamu wa madhehebu ya Shia, Afghanistan

Wakati huo huo, katika mchakato wa kuunda serikali jumuishi, jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Afghanistan inatarajia kuwa itashirikishwa katika masuala mbalimbali ya kiutawala kwa njia ya kiadilifu.

Bila shaka, kujiondoa Taliban kwenye ukiritimba katika masuala mbalimbali kunaweza kuzuia uingiliaji wowote wa duru za kigeni hususan nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya Afghanistan.

Tags