Aug 18, 2023 02:24 UTC
  • Kushindwa siasa za kibeberu za Marekani nchini Afghanistan

Serikali ya kundi la Taliban nchini Afghanistan imesema kuwa njama za wavamizi na madola ya kibeberu zitashindwa tu nchini humo.

Kundi la Taliban limetoa tamko hilo kwa mnasaba wa kuadhimisha mwaka wa pili wa kutimuliwa Marekani nchini humo na kusema kuwa, njama zote za dola hilo la kibeberu zitashindwa tu na hakuna dola lolote vamizi linaloweza kulipigisha magoti taifa la Afghanistan kwa kutumia nguvu za silaha.

Mapambano dhidi ya wavamizi nchini Afghanistan si jambo jipya. Hivyo kundi la Taliban haliwezi kulifanya suala hilo kuwa ni ushindi kwake peke yake. Wananchi wa Afghanistan wana historia ndefu ya kuwashinda na kuwatimua wavamizi wa nchini kwao. Mapambano ya wananchi wa Afghanistan yameshuhudiwa katika karne za 19 na 20 na 21 dhidi ya wavamizi wa nchi yao. Hii ina maana kwamba wananchi wa Afghanistan wanapinga sana uvamizi wa wageni na kamwe hawaruhusu kupandiwa kichwani na maadui.

Umaskini, maradhi, wakimbizi ndiyo matunda ya uvamizi wa madola ya kibeberu Afghanistan

Amin Farhad, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusu suala hilo kwamba: "Ijapokuwa madola ajinabi yanaikodolea macho ya tamaa Afghanistan muda wote, na ijapokuwa Afghanistan ina historia ya kukaliwa kwa mabavu na madola ya kigeni, lakini wavamizi hao wote wamekuwa wakitimuliwa na hawawezi kuikalia kwa mabavu muda wote nchi hiyo."

Ni kwa sababu hiyo ndio maana katika tamko lake, kundi la Taliban limesema, kukombolewa mji mkuu wa nchi hiyo Kabul miaka miwili iliyopita, kwa mara nyingine kumethibitisha kwamba, hakuna mtu yeyote anayeweza kutumia nguvu za dola lolote la kigeni kuwapandia kichwani wananchi wa Afghanistan. Uhakika huo unatokana na dhati ya kiutamaduni, kiustaarabu na kidini ya wananchi wa Afghanistan. 

Wanajeshi wa Marekani walipokimbia Afghanistan miaka miwili iliyopita

Uingereza, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti na mwishowe Marekani na madola ya Magharibi wote wametimuliwa nchini Afghanistan. Hii ni kwa sababu madola hayo hayakuwa na welewa wowote kuhusu utamaduni, dini, mila na desturi za wananchi wa Afghanistan na walikuwa wanadhani kuwa wanaweza kuigeuza Afghanistan kuwa koloni lao. Lakini Afghanistan ni nchi yenye historia ya kuwa na watu muhimu na wakubwa kama Ahmad Shah Masoud ambaye hadi leo vijana wa Afghanistan wanaendelea kumfanya kigezo chao katika mapambano dhidi ya wavamizi.

Alaakullihaal, Jumanne ya tarehe 15 Agosti 2023, ilitangazwa kuwa siku ya mapumziko rasmi nchini Afghanistan kwa mnasaba wa kutimia miaka miwili ya tangu kundi la Taliban kurejea tena madarakani. Sherehe mbalimbali zilifanyika siku hiyo. Lakini kitu ambacho sambamba na sherehe hizo kinawashangaza wananchi wa Afghanistan ni kwamba kwa nini katika wakati wa utulivu na amani, wakuu wa makabila na kaumu tofauti za Afghanistan wanashindwa kukaa pamoja, kushikamana na kushirikiana katika kuliletea maendeleo taifa lao?

Swali hilo tunaweza kuliuliza kwa sura nyingine kwamba, kwa nini Waafghani wanakuwa kitu kimoja katika kupambana na uvamizi wa kigeni lakini baada ya kufanikiwa kuwatimua wavamizi hao, viongozi wa Afghanistan wanasahau kipindi kigumu sana walichokivuka na wanashindwa kuunganisha nguvu zao katika kuliletea maendeleo na ustawi taifa lao? Matokeo yake ni kuzuka uasi na kuanza kupigana wao kwa wao. Wachambuzi wa mambo wanasema, tatizo kubwa la Afghanistan ni ukiritimba wa madaraka unaohodhiwa na kundi fulani tu la watu na kutupwa pembeni watu wengine wa kaumu na mirengo mengine ya kisiasa na kidini. Ugonjwa huo wa kutokubali kushirikiana na wengine katika mdaraka ndiyo sababu kuu inayopelekea kuzuka vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Afghanistan baada ya kutimuliwa madola vamizi. 

Wanajeshi wa Marekani walifika wakati wakawa wanawaongopa hata watoto wadogo wa Afghanistan

Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo pia ndio maana viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao siku chache tu zilizopita walikabidhiwa shukrani rasmi za maandishi na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC kutokana na mchango wao mkubwa wa kutatua mgogoro wa Afghanistan na kupokea maelfu ya wakimbizi wa nchi hiyo, wakawa wanatilia mkazo sana wajibu wa kuundwa serikali kuu itakayowashirikisha watu wa matabaka yote huko Afghanistan. 

Serikali iliyoko madarakani hivi sasa ya kundi la Taliban nchini Afghanistan inapaswa ijufinze kutokana na historia ya nchi hiyo ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kutimuliiwa madola vamizi, na iunde serikali kuu ya umoja wa kitaifa ambayo itawashirikisha watu wa kada na matabaka yote ya Afghanistan kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano na hatimaye kulileta ustawi na maendeleo taifa hilo la Waislamu na kuondoa visingizio vyote vya kuzuka vita vya ndani na uvamizi wa madola ya kigeni.

Tags