Aug 27, 2023 14:21 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Taliban afanya mazungumzo na wabunge wa Iran mjini Kabul

Ujumbe wa wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) walioko ziarani nchini Afghanistan wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Taliban katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul.

Ujumbe wa wabunge hao saba unaoongozwa na Javad Karimi Qudousi umekutana na Amir Khan Motaghi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Taliban, na kuzungumza naye kuhusu masuala yanayohusu maslahi ya pande mbili, ikiwa ni pamoja na usalama, mapambano dhidi ya dawa za kulevya, uzuiaji wa magendo, ulinzi wa mipaka na biashara.
Kwa upande wake, Motaghi amesema: Kutokana na kurejea madarakani kundi la Taliban, ulinzi umeimarishwa nchini Afghanistan na vyombo vya usalama vya nchi hiyo vimeweza kuwamaliza magaidi wa DAESH (ISIS), jambo ambalo lina manufaa si kwa Afghanistan pekee, bali pia kwa nchi za ukanda huu na ulimwengu kwa ujumla.

Wabunge wa Iran katika kikao na waziri wa mambo ya nje wa Taliban

Waziri wa mambo ya nje wa Taliban ameongeza kuwa: Serikali ya mpito ya Taliban imechukua hatua madhubuti katika vita dhidi ya mihadarati; na kilimo cha mpopi kimepungua hadi kiwango cha karibu ya sifuri.
Katika mazungumzo yao na Mtaghi, wabunge wa Iran wamesisitiza juu ya uzuiaji wa magendo, ushughulikiaji wa matatizo ya mipakani na uzuiaji endelevu na wa pamoja wa safari za watu wasio na vibali vya kuingia katika nchi mbili.
Matukio yaliyojiri karibuni nchini Afghanistan yameibua wimbi jipya la raia wa Afghanistan wanaomiminika nchini Iran, na Jamhuri ya Kiislamu, licha ya kukabiliwa na matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na vikwazo vya kidhalimu na bila ya usaidizi wa kimataifa, haikuweka vikwazo vyovyote kwa watu hao kuingia nchini na imekuwa mwenyeji mwema wa kuwakirimu wahamiaji hao.
Uhusiano mzuri kati ya wananchi wa Iran na wa Afghanistan, safari za raia wa Afghanistan kuelekea Iran na kuwepo kwa wahajiri wa Afghanistan nchini Iran kwa zaidi ya miongo minne sasa kumewafanya Waafghanistan waichukulie Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa nchi yao ya pili.../

 

Tags