May 01, 2024 04:05 UTC
  • Kenyatta kuongoza ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika  uchaguzi Afrika Kusini

Umoja wa Afrika (AU) umetangaza kwamba umetuma ujumbe wa waangalizi kufuatilia uchaguzi mkuu ujao nchini Afrika Kusini.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, AU ilisema Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa AU (AUEOM), unaojumuisha waangalizi 60 wa muda mfupi, unaoongozwa na rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, unatazamiwa kuwa mwangalizi wa uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini kuanzia Mei 21 hadi Juni 3.

Taarifa hiyo kwa vyombo vya habari ilisema waangalizi wa Umoja wa Afrika watashirikiana na wadau kadhaa na kuangalia maandalizi ya mwisho na mchakato wa upigaji kura.

Baada ya kukamilika zoezi la upigaji kura,  Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa AU utatoa taarifa yake ya awali baada ya siku ya uchaguzi,"

Uchaguzi wa kitaifa na serikali za mitaa Afrika Kusini umepangwa kufanyika tarehe 29 ya mwezi huu wa Mei.

Kulingana na shirika la usimamizi wa uchaguzi nchini Afrika Kusini, uchaguzi wa 2024 unatarajiwa kuwa wenye ushindani mkubwa katika historia ya nchi hiyo, huku zaidi ya wagombea 14,000 wakiwania viti 887 katika mabunge ya kitaifa.

Hivi karibuni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alipongeza mafanikio ya nchi hiyo chini ya uongozi wa chama chake cha African National Congress (ANC).

"Afrika Kusini leo ipo mahali pazuri zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 30," Ramaphosa alisema katika hotuba yake ya kuadhimisha "Siku ya Uhuru" katika Majengo ya Muungano mjini Pretoria .

Ramaphosa mwenye umri wa miaka 71 alitumia fursa hiyo kuelezea mafanikio na maboresho yaliyofanywa na chama cha ANC, ambacho kinakabiliwa ushindani mkali katika uchaguzi ujao kikiwa katika hatari ya kupoteza kwa mara ya kwanza wingi wa wabunge.