May 01, 2024 04:03 UTC
  • Miili 10,000 iliyozikwa chini ya vifusi vya Gaza, inaoza na kueneza magonjwa

Shirika la Ulinzi wa kiraia la Gaza limeonya kuhusu maafa ya kiafya yanayokuja katika Ukanda uliozingirwa kutokana na kuoza maiti zilizo chini ya vifusi vya majengo yaliyoharibiwa na mashambulizi ya mabomu ya utawala katili wa Israel.

Shirika hilo limetoa taarifa Jumanne na kuonya kuhusu hatari ya magonjwa na milipuko kutokana na kuoza  maelfu ya miili iliyo chini ya vifusi kutokana na kuongezeka kwa joto.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza miezi saba iliyopita na kusababisha hasara kubwa katika Ukanda wa Gaza na inakadiriwa kuwa, kuna miili 10,000 chini ya vifusi.

Nalo shirika la Euro-Mediterranean Human Rights Monitor lenye makao yake mjini Geneva hivi karibuni limeonya kwamba kuoza kwa maiti kwa muda mrefu kunasababisha kuenea kwa magonjwa hatari, ikiwa ni pamoja na virusi vya damu na kifua kikuu.

Kundi la Global Nutrition pia linakadiria kwamba angalau asilimia 90 ya watoto wa Ukanda wa Gaza walio chini ya umri wa miaka mitano wameathiriwa na ugonjwa mmoja au zaidi wa kuambukiza na kwamba, asilimia 70 wameugua kuhara katika wiki mbili zilizopita - ongezeko la mara 23 ikilinganishwa na mwaka 2022.

Jitihada za kufukua miili katika vifusi Gaza

Halijoto isiyotarajiwa kote Gaza pia imeongeza masaibu ya kila siku wanayokabili watu wa eneo hilo na kuzua hofu mpya ya milipuko ya magonjwa huku kukiwa na ukosefu wa maji safi na utupaji taka, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu, pia. inayojulikana kama UNRWA lilisema Alkhamisi.

Haya yanajiri huku idadi ya waliouawa  kutokana na vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza ikiongezeka hadi 34,535. Miongoni mwa waliofariki dunia ni zaidi ya watoto 14,500 na wanawake 9,500.

Aidha tangu vita vilipoanza Oktoba 7, karibu asilimia 85 ya watu milioni 2.3 wa Gaza wameyakimbia makazi yao.