May 01, 2024 04:28 UTC
  • Uingereza yawawekea vikwazo wanasiasa wa Uganda akiwemo Spika wa Bunge

Uingereza imewawekea vikwazo na marufuku ya kusafiri wanasiasa kadhaa wa Uganda akiwemo spika wa bunge la nchi hiyo Anita Among kufuatia madai ya ufisadi.

Serikali ya Uingereza imesema hii ni mara ya kwanza kutumika kwa sheria yake mpya ya kimataifa ya vikwazo dhidi ya ufisadi kwa watu wanaokabiliwa na madai ya ufisadi nchini Uganda, na kwamba ni sehemu ya msako wa kimataifa.

Wanasiasa wengine wa Uganda waliioko katika orodha hiyo ya marufuku ya kusafiri ya Uingereza ni Mary Goretti Kitutu na Agnes Nandutu waliokuwa mawaziri wanaohusika na eneo maskini la mpaka wa Uganda la Karamoja.

Hata hivyo Bunge la Uganda limepuuza hatua hiiyo ya Uingereza na kueleza kwamba, haina msingi wowote.

Taarifa iliyotolewa na bunge la Uganda, mesema vikwazo hivyo vinatokana na kile ilichotaja kuwa dhana potofu.

Bunge la Uganda

 

Taarifa hiyo pia imesema kuwa Among hajawahi kushitakiwa kwa ufisadi katika mahakama yoyote ya kisheria kinyume na dhana inayoibuliwa katika taarifa iliyotolewa na Uingereza.

Bunge la Uganda limebainiisha pia kuwa, madai ya ufisadi yametumiwa kama mbinu ya kuficha sababu halisi ya vikwazo hivyo ambayo haijatajwa lakini iliyo wazi na iliyoitaja kuwa msimamo wake kuhusu sheria ya kupinga ushoga iliyopitishwa hivi majuzi.