May 01, 2024 04:02 UTC
  • Jeshi la Mali latangaza kumuua kinara mkuu wa magaidi eneo la Sahel

Jeshi la Mali limetangaza kumuua mmoja wa vinara wakuu wa magaidi katika eneo la Sahel, magharibi mwa Afrika.

Abu Huzeifa, almaarufu Higgo, aliuawa Jumapili asubuhi wakati wa operesheni katika eneo la Indelimane katika eneo la kaskazini la Menaka karibu na mpaka wa Niger, jeshi lilisema katika taarifa.

Aliwahi kuwa kamanda wa kijeshi wa kundi la kigaidi la Daesh/ISIS, katika Sahel, katika eneo la mpakani mwa Mali-Niger-Burkina Faso.

Jeshi lilisema kuwa Huzeifa alikuwa raia wa kigeni, na ripoti zinaonyesha kuwa, yamkini alikuwa raia wa Morocco. Kundi la Huzeifa liliripotiwa kutekeleza operesheni za kigaidi katika eneo la Menaka nchini Mali, ambako lililaumiwa kwa mashambulizi kadhaa ya kigaidi dhidi ya raia wa Mali.

Burkina Faso, Mali na Niger zinachangia vifo vingi kutokana na ugaidi katika eneo hilo, kulingana na Global Terrorism Index 2024, ripoti iliyochapishwa na Taasisi ya Uchumi na Amani yenye makao yake makuu nchiini Australia .

Nchi hizo tatu zinakabiliwa na ongezeko la ukosefu wa usalama, huku makundi ya kigaidi yenye mafungamano na al-Qaeda na Daesh/ISIS yakihama kutoka Mali kwenda kwa majirani wengine katika eneo la Sahel.

Kwa muda mrefu majeshi ya Ufaransa yalikuwa katika eneo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu na madini ya urani kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi lakini magaidi waliongezeka pamoja na kuwepo askari hao wa Ufaransa. Hivi sasa nchi za eneo la Sahel zimeomba msaada wa Russia katika kupambana na ugaidi na zimeanza kupata mafanikio.