Sep 16, 2023 02:19 UTC
  • Uturuki yafanya mazungumzo na Iraq, Qatar na UAE kuhusu mradi wa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amethibitisha kuwa nchi yake inafanya mazungumzo na Iraq, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) na Qatar kuhusu mradi wa "Barabara ya Maendeleo".

Kwa mujibu wa Kituo cha Habari Cha Middle East News, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan ametangaza kuwa nchi hiyo, Iraq, Imarati na Qatar zinaendelea na mazungumzo ya kina kuhusu mradi wa barabara ya maendeleo.

Barabara ya maendeleo inaanzia mkoa wa Basra kusini mwa Iraq hadi mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo na kuendelea Uturuki na kuiunganisha Asia na Ulaya.

Fidan ameongeza kuwa njia mpya za biashara zimekuwa na umuhimu baada ya mabadiliko ya kijiopolitiki yaliyojiri miaka ya hivi karibuni, likiwemo janga la dunia nzima la Corona, vita vya Ukraine na Russi, na ushindani kati ya Marekani na Magharibi mkabala na China.

Mwanadiplomasia huyo wa Uturuki amebainisha kuwa njia za biashara ni matokeo ya ushindani huo wa kijiopolitiki na akabainisha kuwa mradi wa "Barabara ya Maendeleo" ulizungumziwa pia katika mikutano ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na viongozi walioshiriki katika mkutano wa G20 huko New Delhi, India.

Hakan Fidan

Kwa mujibu wa Fidan, kwa sasa Uturuki inashughulikia mradi huo wa Barabara ya Maendeleo inayoanzia mkoa wa Basra kusini mwa Iraq na kuendelea hadi kaskazini mwa nchi hiyo na kisha kuunganishwa na Uturuki na hatimaye kuiunganisha Asia na Ulaya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameeleza kuwa Iraq, Muungano wa Falme za Kiarabu, Uturuki na Qatar zinafanya mazungumzo ya kina katika uwanja huo, na kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na mwenzake wa Imarati, Mohammad Bin Zayed Al Nahyan, ubunifu wa mradi huo utakamilika rasmi mnamo miezi michache ijayo.

Tarehe 22 Agosti, wakati wa safari yake nchini Iraq, Fidan alitangaza utayari wa Uturuki kushiriki katika miradi ya maendeleo nchini Iraq, hasa mradi wa Barabara ya Maendeleo.

Inafaa kuashiria kuwa mradi wa Barabara ya Maendeleo, ambayo inaiunganisha Asia na Ulaya kupitia Iraq kwa barabara na njia ya reli zenye urefu wa kilomita 1200 ulizinduliwa nchini humo mwezi wa Mei mwaka huu.../

 

Tags