Waandishi wa habari; wahanga wa usimuliaji ukweli kuhusu jinai za Wazayuni
Katika vita vilivyoanzishwa na Wazayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza, hadi sasa waandishi wa habari 73 wameshauawa shahidi kutokana na mashambulio ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni.
Waandishi wa habari waliouawa shahidi walikuwa na uraia wa nchi tofauti zikiwemo Palestina, Lebanon na Uturuki. Siku ya Ijumaa pekee, ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya vita baada ya kumalizika usitishaji mapigano wa siku saba, waandishi wa habari watatu waliuawa shahidi. Muntaser Mustafa Al-Sawaf na Marwan Al-Sawaf, ndugu wawili waliokuwa wanahabari wa Shirika la Habari la Anatolia la Uturuki, na Abdullah Darwish, mpiga picha na ripota wa televisheni ya Al-Aqsa, ni wanahabari watatu waliouliwa shahidi siku hiyo.

Wakati madola yanayodai kutetea uhuru na haki za binadamu yamenyamazia kimya kuuliwa shahidi waandishi wa habari 73, baadhi ya watu na asasi kadhaa zimeguswa na hivyo kuamua kutoa mjibizo kwa jinai hiyo ya Wazayuni. Mick Wallace, mbunge wa Ireland katika Bunge la Ulaya, ameweka ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X usemao: "serikali ya ubaguzi wa rangi wa Apathaidi ya Israel inawalenga waandishi wa habari wanaoonyesha ujasiri wa kufichua uhalifu wake wa kivita." Jumuiya ya Maripota Wasio na Mipaka imesema, tangu mwaka 2001 utawala wa Kizayuni umeshaua makumi ya waandishi wa habari na haujawajibika kwa suala hilo na kueleza kwamba, viongozi wa Kizayuni hawana nia ya kuwapa ulinzi waandishi wa habari na kimsingi, wanawalenga kwa makusudi.
Jumuiya hiyo ya maripota wasio na mipaka imebainisha kuwa, kukataa utawala wa Kizayuni kuwapa ulinzi waandishi wa habari kumekuwa sababu ya kuteketea roho za waandishi wa habari walioko Gaza. Anthony Belanger, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Kimataifa la Wanahabari, ametangaza kwamba kinachotokea dhidi ya waandishi wa habari, wanawake na watoto huko Gaza ni mashambulizi ya kuwalenga watu kwa makusudi.
Lakini licha ya mtazamo na muelekeo huo wa nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni kuhusiana na waandishi wa habari, jinai za Wazayuni hazijaweza kufichika; na maoni ya umma ulimwenguni yamejipanga pamoja na kusimama dhidi ya utawala huo mtenda jinai na muuaji wa watoto. Katika taarifa iliyotoa kuwaunga mkono waandishi wa habari, harakati ya HAMAS imesema: "Sera ya kuwaua na kuwateketeza waandishi wa habari kamwe haitaweza kupelekea kufichika ukweli wa jinai za Kinazi za Wazayuni dhidi ya watoto na wanawake na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huu unaopata uungaji mkono wa moja kwa moja wa Rais Joe Biden wa Marekani na serikali yake ya Kizayuni".../