Jan 21, 2024 11:26 UTC
  • Wanamuqawama wa Iraq wakishambulia kituo cha jeshi la Marekani kwa maroketi na makombora 40

Vikosi vya Muqawama wa Iraq vimekishambulia kwa maroketi na makombora 40 kituo cha wanajeshi vamizi wa Marekani cha A'inul-Assad kilichoko kwenye mkoa wa Al-Anbar.

Kamandi Kuu ya Kijeshi ya Marekani (CENTCOM) imetoa taarifa iliyothibitisha kufanyika shambulio la makombora lililolenga kambi ya A'inul-Assad na kueleza kwamba: kufuatia shambulio la makombora na maroketi lililofanywa na Muqawama wa Iraq dhidi ya kambi ya A'inul-Assad magharibi mwa Iraq, wanajeshi kadhaa wa Marekani wamefanyiwa uchunguzi kuona kama wameathirika ubongo.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutajwa jina lake, makombora kadhaa ya balestiki (TBM) yametumiwa katika shambulio la vikosi vya Muqawama wa Iraq dhidi ya kituo cha kijeshi cha A'inul-Assad.

Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umetoa taarifa kuthibitisha kwamba ndio uliohusika na shambulio la makombora lililolenga kambi ya kijeshi ya Marekani huko A'inul-Assad.

Kufuatia mashambulio ya kinyama na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza na uungaji mkono wa Washington kwa mashambulizi hayo, makundi ya muqawama ya Iraq yameionya Marekani kwamba yatavishambulia vituo vya nchi hiyo katika eneo.

Halikadhalika katika taarifa yake, Muqawama wa Kiislamu wa Iraq umesisitiza kuwa utaendelea kuzishambulia ngome  na vituo vya vikosi vya jeshi vamizi la Marekani.../

 

 

Tags