Feb 07, 2024 05:56 UTC
  • Qatar: Hamas imetoa jibu chanya kwa mpango wa Gaza wa kufikia mapatano ya kusitisha vita

Waziri Mkuu wa Qatar amesema Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa "jibu chanya" kuhusiana na uwezekano wa kufikia usitishaji vita mpya katika Ukanda wa Gaza na kubadilishana mateka kati yake na utawala wa Israel.

Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani Waziri Mkuu wa Qatar  amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa nchi hiyo Doha akiwa pamoja na Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwamba jibu la Hamas linajumuisha pia maelezo lakini kiujumla ni chanya.  

Waziri Mkuu wa Qatar ameashiria kupiga hatia mazungumzo yao hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu kilichojadiliwa. Amesema wanachotaka ni kufikiwa makubaliano haraka iwezekanavyo kwa kushirikiana na washirika wao huko Cairo na Washington. Amesema, vita katika Ukanda wa Gaza ni lazima vimalizike na akaongeza kuwa hawataki vita hivyo vienee katika eneo zima au kuwa tishio kwa usafiri baharini kimataifa. 

Vita vya utawala wa Kizayuni Ukanda wa Gaza 

Itakumbukwa kuwa, katika usitishaji vita wa wiki moja uliofikiwa na Hamas na utawala wa Kizayuni mwezi Novemba mwaka jana karibu nusu ya mateka wa utawala wa Kizayuni waliachiwa huru mkabala wa kuachiwa huru wafungwa wa Palestina 240. 

Wapalestina zaidi ya 27,000 wameuliwa shahidi na wengine zaidi ya elfu 67 wamejeruhiwa tangu utawala wa Kizayuni uanzishe vita dhidi ya Ukanda wa Gaza mwezi Oktoba mwaka jana huku asilimia 85 ya wakazi wa eneo hilo wapatao milioni 2.3 wakibaki bila makazi.

Tags