Apr 06, 2024 02:39 UTC
  • Netanyahu ashikilia msimamo wake wa kupinga kuundwa nchi huru ya Palestina

Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amerudia tena msimamo wake wa kupinga katakata kuundwa nchi huru ya Palestina alipokutana na ujumbe wa Marekani wa wabunge wa chama cha Republican.

Ujumbe huo unatembelea ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu iliyopandikizwa jina bandia la Israel, kwa niaba ya kundi na lobi ya Kizayuni ya nchini Marekani inayoiunga mkono Israel ya American Israel Public Affairs Committee (AIPAC).
 
Netanyahu amedai katika mazungumzo na ujumbe huo kwamba, kuna jaribio la kulisakamiza dola la Palestina kwenye koo zao.
 
Katika mazungumzo hayo, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni amedai pia kuwa nchi ya Palestina itatumika kama kimbilio jingine la ugaidi na njia nyingine ya kuanzishia mashambulizi, kama ilivyokuwa kwa alichokiita 'nchi' ya Hamas huko Ghaza.

Netanyahu ameendelea kusema eti Waisraeli waliowengi wanapinga jambo kama hilo.

 
Wakati huohuo Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, bado hakuna hatua iliyopigwa katika mazungumzo yasiyo ya ana kwa ana kati yake na utawala wa Kizayuni wa Israel juu ya mpango wa kusitisha mapigano, kwa sababu Tel Aviv "haijabadilika," na imekataa kila pendekezo ambalo limetolewa.

Mazungumzo hayo ambayo yanafanyika kwa uunganishi wa Misri na Qatar na kwa uungaji mkono wa Marekani, yanalenga kufikia mapatano ili kubadilishana na kuachiliwa mateka waliosalia, ambao wanashikiliwa na Hamas tangu ilipofanyika operesheni ya Kimbunga cha Al- Aqsa dhidi ya Israel Oktoba 7,2023.../

Tags