May 06, 2024 02:33 UTC
  • Kiongozi wa HAMAS: Makubaliano ya usitishaji vita lazima yakomeshe uchokozi wa utawala wa Israel

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kuwa, harakati hiyo inataka kufikia makubaliano kamili na jumuishi ili kukomesha uchokozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni.

Ismail Haniya alitangaza jana Jumapili kwamba ujumbe wa Hamas katika mazungumzo ya Cairo umesimama thabiti katika misimamo yake chanya na inayojadilika kwa kujikita kwenye kipaumbele cha kusimamisha hujuma za utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, kuhakikisha vikosi vya utawala huo haramu vinaondoka huko Ghaza na kutekelezwa zoezi la kubadilishana mateka.
Haniya ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni mfanya mauaji ya kimbari umeigeuza dunia kuwa mateka wake na kuzusha matatizo mengi ya kisiasa, mbali na kufanya jinai za kutisha katika Ukanda wa Ghaza.
Mkuu wa harakati ya Hamas amesema, Marekani, ambayo inauunga mkono utawala wa Kizayuni inapaswa iuzuie na kuudhibiti utawala huo mfanya mauaji ya kimbari badala ya kuutayarishia silaha za maangamizi.

Siku ya kwanza ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza ilimalizika jana Jumapili katika mji mkuu wa Misri, Cairo bila kufikiwa makubaliano yoyote.

Mjumbe wa Hamas, Mahmoud Mardawi alisema siku ya Jumamosi kuhusu mazungumzo ya Cairo kwamba wawakilishi wa harakati hiyo wamekwenda kwenye mazungumzo mji mkuu wa Misri wakiwa na hali na mtazamo chanya, lakini kilichowasilishwa mjini Cairo ni pendekezo tu na si mwongozo wa kufikia mwafaka.
Mjumbe huyo wa Hamas amebainisha kuwa Hamas inasisitiza kurejea kwa wakimbizi, kujengwa upya kwa Ukanda wa Ghaza na kuondoka kikamilifu wavamizi katika ukanda huo.../

 

Tags