Dec 24, 2020 03:30 UTC
  • Jihad al Islami: Shahid Soleimani alikuwa mhandisi wa kambi ya muqawama

Kiongozi mmoja mwandamizi wa harakati ya Jihad al Islami ya Palestina amesema kuwa, shahid Qassem Solaimani ndiye hasa aliyeyaimarisha makundi yote ya muqawama katika eneo hili.

Khalid al Batsh alisema hayo jana (Jumatano) na kuongeza kuwa, shahid Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran SEPAH, ndiye aliyeyaimarisha makundi yote ya muqawama. Ametoa mifano ya makundi hayo akisema kuwa ni pamoja na Brigedi za Quds ambalo ni tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na Brigedi za Qassam ambalo ni tawi la kijeshi la Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina pia. Mengine amesema ni Brigedi za Mashahidi wa al Aqsa katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na makundi mengine kama Abu Ali al Mustafa, al Wilaya al Naasir, Hizbullah na matawi mengine yote ya kijeshi ya makundi ya wanamapambano wa Kiislamu katika eneo hili.

Shahid Qassem Soleimani

 

Kiongozi huyo muhimu wa harakati ya Jihad al Islami ya Palestina vile vile amesema, shahid Soleimani alikuwa mhandisi bingwa wa kambi ya muqawama na ndio maana hata Wamarekani walikuwa wanakiri nafasi yake muhimu sana katika medani za kupambana na adui Mzayuni-Mmarekani na uungaji mkono wake kwa muqawama wa Palestina.

Ameongeza kuwa, kitendo cha kijinai na kigaidi cha Marekani cha kumuua kidhulma mwanamapambano hayo pamoja na wanamapambano  wengine wa muqawama wa Lebanon, Palestina na kwengineko kamwe hakiwezi kukwamisha mapambano ya mashujaa wa eneo hili.

Tags