Jan 08, 2021 07:04 UTC
  • Wairaq wafurahishwa na waranti wa kusakwa Trump ili akajibu mashtaka ya mauaji

Katibu Mkuu wa "Kataib al Shuhada" ya Iraq ameipongeza idara ya mahakama ya nchi hiyo kwa kutoa waranti wa kutiwa mbaroni rais wa Marekani, Donald Trump ili akajibu mashtaka ya kuwaua kidhulma kamanda Qassem Soleimani na Abou Mahdi al Muhandis ndani ya ardhi ya Iraq.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Abu Ala al-Walai Katibu wa Kataib al Shuhada ya Iraq, jana Alkhamisi alitumia mtandao wa kijamii wa Twitter kuipongeza idara ya mahakama ya nchi hiyo kwa kutoa waranti wa kutiwa mbaroni wauaji waovu kabisa waliomwaga damu za watu wema kabisa ndani ya ardhi ya Iraq.

Naye Mbunge Riyadh al Masoud wa muungano wa Sairun katika bunge la Iraq amesema kuwa, amri ya kutiwa mbaroni rais wa Marekani, Donald Trump imepangwa kutekelezwa ndani ya Iraq, kwa maana ya kwamba wakati wowote Trump atakapokanyaga ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu, atatiwa mbaroni.

Abu Ala al-Walai

 

Kwa upande wake, Tariq Harb, mtaalamu wa masuala ya sheria wa Iraq amesema, hukumu ya kutiwa mbaroni Trump ni ya kisheria na hiyo ni moja ya njia za kuhakikisha mtuhumiwa anapandishwa kizimbani. Jaji maalumu wa mahakama ya al Raswafa ambayo ndiyo inayofuatilia mashtaka ya jinai iliyofanywa na Marekani dhidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu Taasisi ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi, ndiye aliyetoa waranti wa kutiwa mbaroni rais wa Marekani, Donald Trump.

Wanajeshi magaidi wa Marekani waliwaua kidhulma shahid Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis pamoja na wanamapambano wenzao wanane tarehe 3 Januari 2020 karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad mji mkuu wa Iraq kwa amri wa rais wa Marekani, Donald Trump. Damu ya mashahidi hao itaendelea kuwaandama milele watenda jinai hao wakiongozwa na Donald Trump.

Tags