Jul 08, 2022 10:31 UTC
  • Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Allah wasimama Arafa

Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu wanasimama katika uwanja wa Arafa hii leo Ijumaa, kisimamo hicho kikiashiria kilele cha ibada tukufu ya Hijja.

Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na Mlima wa Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingi za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.

Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SWT ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hijja na ameweka meza na karamu yake pembeni ya Jabalur Rahma.

Magharibi ya siku hii ya leo Mahujaji wataondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hijja, kama kulala Muzdalifa, na kufanya amali ya Jamarat (kumpiga shetani kwa mawe saba) Jumamosi.

Waislamu katika Msikiti Mtukufu wa Makka

Waislamu milioni moja wakiwemo raia wa kigeni 850,000 wamekusanyika katika mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya Hijja ya mwaka huu, ikiashiria hatua kubwa kuelekea hali ya kawaida baada ya miaka miwili ya janga la corona ambapo idadi ya Mahujaji ilipunguzwa sana.

Hata hivyo idadi hii bado ni ndogo ikikumbukwa kuwa, kabla ya janga la corona Waislamu milioni 2.5 waliweza kutekeleza nguzo hiyo muhimu ya Uislamu  mwaka  2019.

Tags