Jun 20, 2023 03:14 UTC
  • Qatar na Imarati zarejesha uhusiano kamili wa kidiplomasia, mabalozi wa pande mbili waanza kazi

Qatar na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) zimetangaza kurejesha kikamilifu uhusiano wao wa kidiplomasia na tayari mabalozi wa pande hizo mbili wameanza kazi.

Shirika la Habari la Qatar (QNA) limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, ubalozi wa Qatar huko Abu Dhabi na ubalozi wake mdogo wa mjini Dubai, pamoja na ubalozi wa Imarati mjini Doha zilianza tena kazi rasmi jana Jumatatu. 

Pande zote mbili zimesisitiza kuwa hatua hiyo muhimu inaakisi azma ya viongozi wa nchi zote mbili ya kurejesha uhusiano wao kama zamani na itachangia kuendeleza mipango ya pamoja ya nchi za Kiarabu ya kutimiza matarajio ya wananchi wa nchi hizo ndugu.

Viongozi wa Qatar na Imarati katika mazungumzo ya ana kwa ana

Mwezi Juni 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilitangaza kukata uhusiano wao wote na Qatar na kuiwekea vikwazo vya kila upande vya angani, baharini na ardhini nchi hiyo. Raia na wanadiplomasia wa Qatar waliokuweko kwenye nchi hizo nne za Kiarabu walitimuliwa kijeuri na hivyo kukazuka mgogoro mkubwa katika Ulimwengu wa Kiarabu. Nchi hizo zilidai kuwa zimechukuwa hatua hiyo dhidi ya Qatar kwa kile walichoiita kuunga mkono ugaidi na kuvuruga utulivu wa eneo hilo, madai ambayo Qatar iliyakanusha vikali.

Baada ya kuona mashinikizo na vikwazo vyao vimeshindwa kupigisha magoti Qatar, mwaka 2021, Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zilitangaza kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Doha. Zilitangaza hayo pambizoni mwa Mkutano wa 41 wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi uliofanyika Al-Ula, Saudi Arabia.

Lakini mchakato wa kurejeshwa rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Qatar ulichereweshwa kutokana na kukosekana maafikiano kuhusu masuala fulani fulani.

Tags