Putin asisitiza udharura wa kuwepo msimamo mmoja katika kupambana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i28342-putin_asisitiza_udharura_wa_kuwepo_msimamo_mmoja_katika_kupambana_na_ugaidi
Rais Vladmi Putin wa Russia amesema katika ujumbe uliosomwa kwenye Mkutano wa Sita wa Usalama wa Kimataifa mjini Moscow kwamba, mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika yanahitaji kuwa na mtazamo na msimamo mmoja na unaooana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 27, 2017 21:58 UTC
  • Putin asisitiza udharura wa kuwepo msimamo mmoja katika kupambana na ugaidi

Rais Vladmi Putin wa Russia amesema katika ujumbe uliosomwa kwenye Mkutano wa Sita wa Usalama wa Kimataifa mjini Moscow kwamba, mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika yanahitaji kuwa na mtazamo na msimamo mmoja na unaooana.

Mkutano wa Sita wa Usalama wa Kimataifa wa Moscow ulianza Jumatano ukihudhuriwa na wajumbe kutoka nchi karibu 80 katika mji mkuu wa Russia. Putini anasema mkutano huo una ajenda na masuala muhimu yanayohitajia mweleleko na msimamo mmoja. Miongoni mwa masuala hayo ni mapambano dhidi ya ugaidi ambao ni tishio kubwa zaidi kwa usalama wa kikanda na kimataifa na suala la kutafuta ufumbuzi wa kisiasa na kidiplomasia wa migogoro na mapigano yanayojiri sasa katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan maeneo ya Mashariki ya Kati ya kaskazini mwa Afrika. 

Magaidi wa Daesh wakichoma moto wahanga wao

Sisitizo hilo la Rais wa Russia juu ya kupambana na ugaidi limetolewa wakati dunia, ikiwemo Russia yenyewe, ikiendelea kukabiliwa na tishio la janga hilo. Kwa hakika shambulizi la kigaidi lililofanyika hivi karibuni katika mji wa St. Petersburg limewakumbusha tena maafisa wa ngazi za juu Russia kwamba, ugaidi wa kitakfiri si tukio la muda na la kupita tu bali ni ishio halisi na linaloongezeka siku baada ya siku.

Vladimir Putin 

Kwa muda sasa Rusia imekuwa ikipambana na makundi ya kigaidi na kitakfiri ndani ya nchi hiyo hususan katika maeneo ya Kaukazia Kaskazini. Makundi hayo yamefanya mashambulizi mengi ndani ya ardhi ya Russia na kuua raia wasio na hatia. Vilevile magaidi wenye misimamo ya kukufurusha Waislamu wengine wanaorejea katika nchi zao wakitokea Syria na Iraq, mbali na masuala ya kiaidiolojia, wana ujuzi wa kivita na kijeshi unawafanya kuwa hatari si kwa Russia pekee bali pia nchi nyingine za Asia ya kati na Kaukazia.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana viongozi wa Russia wanasisitiza kuwa, vitisho vya magaidi hao wenye misimamo ya kufuruta mipaka vinaimarika na kuongeza kila uchao na kwamba, kuna haja ya kuwepo mtazamo mmoja, mshikamano na msimamo madhubuti wa pande zote kwa ajili ya kuweza kung'oa mizizi ya uovu na tishio hilo. Ni kwa sababu hiyo pia ndiyo maana Vladimir Putin, kama kiongozi wa nchi ya Euro-Asia, akatahadharisha katika ujumbe wake, juu ya hatari ya magaidi hao na kutoa wito wa kuwepo mshikamano kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo.  

Pamoja na hayo, tunapaswa kukumbusha hapa kwamba, mapambano ya ugaidi na misimamo mikali yanapaswa kufanyika kimsingi na kwa kupambana na vyanzo na sababu zake, la sivyo tutakuwa tunapambana na sura ya kijujuu tu ya ugaidi na si kutaka kung'oa mizizi yake. Miongozi wa sababu na mizizi ya ugaidi, mbali na sababu za kiaidiolojia na kifikra, ni tabia na mienendo ya kindumakuwili katika kukabiliana na uovu huo. Matukio ya baada ya harakati ya wananchi katika ulimwengu wa Kiarabu hapo mwaka 2011 yalipelekea kujitokeza mazingira ya kustawi na kukua makundi ya kigaidi. Suala hilo linaoenekana waziwazi hususan huko Syria ambayo imefanywa medani ya makundi ya kigaidi na harakari za kitakfiri kama Daesh na Jabhatu Nusra.

Magaidi wa kundi la Daesh

Hata hivyo nchi za Magharibi na washirika wao wa Kiarabu wanayatumia makundi hayo hayo ya kitakfiri na kigaidi kwa ajili ya kutimiza malengo yao badala ya kukabiliana nayo. Katika mkondo huo nchi za Magharibi hususan Marekani, Uingereza na Ufaransa zimekuwa zikiyasaidia kwa hali na mali makundi hayo ya kigaidi, suala ambalo limepekea kupanuka zaidi harakati za makundi hayo na kushindwa kudhibitiwa.

Kwa msingi huo inaonekana kuwa, hatua ya kwanza kabisa ya kupambana ipasavyo na ugaidi ni kuwapo msimamo mmoja wa nchi zote katika katambua hatari ya makundi hayo na ulazima wa kukusanya pamoja nguvu na suhula zote kwa ajili ya kuyaangamiza. Hata hivyo suala hilo linaonekana gumu katika mazingira ya sasa maadamu baadhi ya nchi kubwa zinayaona maslahi yao kuwa yamo katika kuyaunga mkono na kuyasaidia makundi hayo.