Ukosoaji wa Wapalestina kwa utendaji dhaifu wa UNRWA
https://parstoday.ir/sw/news/uncategorised-i3487-ukosoaji_wa_wapalestina_kwa_utendaji_dhaifu_wa_unrwa
Ali Baraka, mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS nchini Lebanon amekosoa utendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kuhusiana na wananchi wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2016 00:20 UTC
  • Ukosoaji wa Wapalestina kwa utendaji dhaifu wa UNRWA

Ali Baraka, mwakilishi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu wa Palestina HAMAS nchini Lebanon amekosoa utendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) kuhusiana na wananchi wa Palestina.

Ali Baraka ameongeza kuwa UNRWA liliasisiwa kwa lengo la kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina katika maeneo mbalimbali hadi watakaporejea kwenye ardhi zao za asili. Miaka 68 imepita tangu tukio la Nakba, siku ilipovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina na Wazayuni huku sehemu kubwa ya raia wa Palestina wakiwa wangali wanaishi katika hali ya ukimbizi nje ya wat'ani na ardhi walikozaliwa.

Mwakilishi wa HAMAS nchini Lebanon amebainisha kuwa kupunguzwa utoaji huduma wa UNRWA au kusitishwa moja kwa moja shughuli za shirika hilo la Umoja wa Mataifa ni njama dhidi ya wakimbizi wa Kipalestina na taifa la Palestina.

Miaka 67 iliyopita, yaani tarehe 8 Desemba mwaka 1949 Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) liliundwa kulingana na azimio nambari 302 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa madhumuni ya kutoa misaada ya moja kwa moja kwa wakimbizi na waomba hifadhi wa Kipalestina, na ili kuwaepusha na baa la njaa, dhiki na shida zilizowakabili na kupeleka mbele mchakato wa amani na uthabiti ili kuweza kuwashughulikia wakimbizi hao.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa kuwafanya wakimbizi na kuwabakisha bila makaazi Wapalestina kwa lengo la kuimarisha nafasi ya utawala wa Kizayuni katika maeneo unayoyakalia kwa mabavu na kuuzatiti utambulisho wa kibaguzi wa utawala huo imekuwa ndio ajenda kuu inayofanyiwa kazi na utawala bandia wa Kizayuni tangu ulipoasisiwa.

Matokeo ya siasa za kinyama za utawala wa Kizayuni yamekuwa ni kuwafanya wakimbizi mamilioni ya Wapalestina ambao idadi yao inakadiriwa kufikia milioni sita.

Sehemu kubwa ya wakimbizi wa Kipalestina wanaishi kwenye kambi mbalimbali zilizoko ndani au nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Tab'an idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Kipalestina wanaishi katika nchi za Kiarabu wakiwemo maelfu miongoni mwao walioko kwenye kambi za wakimbizi katika nchi za Syria na Lebanon.

Hali za wakimbizi hao ni mbaya kiasi kwamba Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeshatoa tahadhari mara kadhaa juu ya suala hilo.

Na hii ni katika hali ambayo ufumbuzi wa suala la wakimbizi wa Kipalestina ni kuwaandalia wananchi wa Palestina mazingira ya kurejeshewa haki zao walizoporwa ikiwemo kupatiwa makaazi na kuishi katika ardhi zao za asili na kuhitimishwa ukaliaji wa mabavu wa utawala wa Kizayuni kama ilivyosisitizwa na maazimio mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.

Azimio nambari 194 la Umoja wa Mataifa limesisitizia haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea kwenye wat'ani na ardhi walikozaliwa pamoja na kulipwa fidia. Kwa hivyo upuuzaji wa jumuiya za kimataifa kuhusiana na haki za Wapalestina ikiwemo haki ya wakimbizi na kuendelea uzembeaji wa jumuiya hizo juu ya suala hilo ndio unaowafanya walimwengu waendelee kushuhudia ongezeko la wakimbizi wa Kipalestina siku baada ya siku na kushadidi mateso na masaibu yanayowapata wakimbizi hao.

Katika hali na mazingira hayo, mnamo miezi ya hivi karibuni UNRWA limetangaza kuwa kutokana na kupungua misaada ya kimataifa iliyoahidiwa kutolewa, na kutodhaminiwa bajeti ya fedha na nchi zilizoahidi kudhamini bajeti hiyo, shirika hilo halina uwezo tena wa kutekeleza majukumu liliyopewa.

Inafaa kuashiria kuwa kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, nchi nyingi za Magharibi na hasa Marekani inakwepa kutekeleza ahadi na wajibu wake kuhusiana na shirika la UNRWA kwa kufungamanisha kuendelea kutoa misaada hiyo na sharti la kusalimu amri Wapalestina mbele ya matakwa haramu ya Magharibi na utawala wa Kizayuni.

Kwa kutupia jicho matukio yanayojiri Palestina tunaweza kuthubutu kusema kuwa kuna njama inayotekelezwa kimataifa ikiongozwa na madola ya Magharibi na hasa Marekani kwa lengo la kukanyaga haki za wakimbizi wa Kipalestina; suala ambalo limeamsha wimbi la lawama na ukosoaji wa Wapalestina.../