May 04, 2016 04:06 UTC
  • Kuongezeka hatua za chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa

Kamisheni ya Mashauri ya Haki za Binadamu nchini Ufaransa (CNCDH) imetangaza katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka mara tatu nchini humo katika mwaka uliopita wa 2015.

Ripoti hiyo ya kila mwaka kuhusiana na vita dhidi ya ubaguzi na hatua nyingine za chuki inasema kuwa, takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa zinaonesha juu ya kuongezeka vitendo vya siri vyenye msukumo wa ubaguzi.

Ripoti ya Kamisheni ya Mashauri ya Haki za Binadamu nchini Ufaransa inaonesha kuwa, vitendo hivyo viliongezeka kwa asilimia 22 mwaka 2014 na asilimia 34 katika mwaka uliopita wa 2015. Aidha ripoti hiyo inafichua kwamba, hatua za chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka kwa asilimia 223. Ripoti hiyo inachanganua kwa kubainisha kwamba, katika mwaka 2015 vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa viliongezeka mara tatu yaani kesi 429 ikilinganishwa na kesi 133 za matukio na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini humo katika mwaka wa kabla yake yaani 2014.

Kabla ya hapo pia, Bernard Cazeneuve Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa alikuwa amekiri juu ya kushadidi vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu katika mwaka uliopita.

Ukweli wa mambo ni kuwa, vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa vilishadidi zaidi baada ya mashambulio ya kigaidi ya Novemba 13 mwaka jana mjini Paris yaliyopelekea watu 132 kuuawa ambapo kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kwamba, ndilo lililohusika na jinai hiyo.

Tukio la hivi karibuni kabisa dhidi ya Uislamu ni lile la siku ya Ijumaa ambapo watu wasiojulikana wealiuchoma moto msikiti katika mji wa Ajaccio katika kisiwa cha Corse. Msikiti huo mwishoni mwa mwaka jana ulishambuliwa na kuchomwa moto pia na watu wasiojulikana.

Katika radiamali yake ya kuchomwa moto msikiti huo, Rais Francosi Hollande wa nchi hiyo sanjari na kutangaza kufungamana kwake na Waislamu wa eneo hilo alitoa amri ya kusakwa na kupandishwa kizimbani haraka iwezekanvyo wale wote waliohusika na kitendo hicho.

Ufaransa kwa kuwa na idadi ya Waislamu zaidi ya milioni sita imekuwa ndiyo nchi yenye jamii kubwa zaidi ya Waislamu barani Ulaya. Pamoja na hayo kiwango cha taasubi, chuki na ubaguzi wa wananchi wa Ufaransa dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo sio tu kwamba, hakijapungua bali kimekuwa kikiongezeka kila mwaka. Katika upande mwingine licha ya kuweko nia njema inayooneshwa na Uislamu wa Ufaransa na licha ya kuweko madai ya kuwaunga mkono Waislamu, lakini jamii ya Waislamu nchini humo imekuwa ikikabiliwa na miamala ya kidhulma na kibaguzi na viongozi, wananchi na hata vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Kuendelea mwenendo wa chuki dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa kumepelekea kuongezeka ukosoaji wa asasi za kutetea haki za binadamu ikiwemo kamati ya kupambana na ubaguzi ya Umoja wa Mataifa; kiasi kwamba, kamati hiyo imeutathmini ubaguzi nchini Ufaransa kuwa ni hatari mno.

Hivi karibuni pia wataalamu wa Baraza la Ulaya walitoa ripoti na kuelezea wasiwasi walio nao kuhusiana na kuendelea matamshi na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa.

Tags