Hamas: Tutalipiza kisasi cha damu ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa italipiza kisasi cha damu ya watoto wa Kipalestina waliouawa shahidi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hamas imetoa taarifa hiyo baada ya wanajeshi wa Israel kumpiga risasi na kumuua shahidi kijana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 15, Muhammad Farid Shawqi Al-Zaarir, jana Jumatano karibu na mji wa Al-Samou kusini mwa mji wa Al Khalil.
Sambamba na kutoa mkono wa pole kutokana na kuuawa shahidi kijana huyo wa Kipalestina na kusisitiza kuwa, hivi karibuni wapiganaji wa Palestina watajibu jinai za wavamizi dhidi ya wananchi wa Palestina, harakati ya Hamas imetangaza kuwa, wanamapambano wa Palestina watarejesha haki za watu wa taifa hilo, ikiwa ni pamoja na kuikomboa Palestina, kuwarejesha nyumbani wakimbizi wote, na kuwarejeshea maisha ya heshima.
Harakati za ukombozi wa Palestina zilitangaza baada ya kuuawa shahidi kijana huyo kwamba, zitalipiza kisasi cha damu ya "Muhammad Farid Shawqi Al-Zaarir" kutoka kwa Wazayuni magaidi.