Mamilioni wakumbuka siku ya kuuawa shahidi Imam Ali (as) kote duniani
Mamilioni ya Waislamu husuan wapenzi na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kote duniani kuanzia jana usiku hadi leo wameshiriki katika majlisi, vikao na mijumuiko ya kukumbuka tukio chungu la kufa shahidi Amiri wa Waumini, Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Majlisi za maombolezo ambazo ziliambatana na ibada za kuhuishausiku wa Lailatul Qadr, zilifanyika kote duniani jana usiku na vikao hivyo vimeendelea leo kwa kukumbuka Bwana wa Wachamungu, Ali bin Abi Twalib (as).
Huko Iraq Idara ya Haram ya Imam ya Imam Ali (as) katika mji mtakatifu wa Najaf imetangaza kuwa, zaidi ya Waislamu milioni tano walishiriki katika shughuli ya maombolezo na kukumbuka tukio hilo chungu lililotokea mwaka 40 Hijria. Afisa wa idara hiyo, Ali al Husseini amesema takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu waliokwenda kufanya ziara katika mji wa Najaf kwa ajili ya kushiriki kumbukumbu ya maombolezo ya Imam Ali (as) mwaka huu imepita watu milioni tano.
Wakati huo huo mkuu wa mkoa wa Najaf, Luayy al Yasiri amesema kuwa usalama umeimarishwa katika mji huo mtakatifu na kwamba walinda amani zaidi ya elfu 23 kutoka jeshi na polisi ya Iraq na vilevile makundi ya kujitolea na wananchi, wanasimamia amani katika mji huo.
Majlisi za kukumbuka tukio chungu la kuuliwa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib pia zinaendelea katika pembe mbalimbali za dunia.
Hapa nchini Iran mamilioni ya waumini wameshiriki katika shughuli hiyo katika miji mbalimbali na shughuli zote za umma zimefungwa leo kwa ajili ya kuenzi na kumkumbuka Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).
Imam Ali bin Abi Twalib (as) alikufa shahidi tarehe 21 Ramadhani mwaka 40 Hijria siku mbili baada ya kupigwa upanga utosini na mtu aliyejulikana kwa jina la Ibn Muljim akiwa katika ibada ya Swala msikitini.