Jeshi la Iran launga mkono Intifadha ya Palestina
Kamandi ya Majeshi yote ya Iran imetoa wito kwa watu wote katika ulimwengu wa Kiislamu kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds Ijumaa hii.
Katika taarifa yake iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds, Kamandi ya Majeshi yote ya Iran imesema, ubunifu wa kistratijia wa Imam Khomeini MA, katika kuitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni fursa kwa ajili ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ungali changamoto kubwa katika Umma wa Kiislamu.
Wakati huo huo, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, Ali Larijani amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu taifa la Palestina katika mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni."
Larijani ameyasema hayo leo Jumanne mjini Tehran wakati alipokutana na wanaharakati kadhaa wanaohusika na mapambano ya kuikomboa Quds Tukufu na Palestina kutoka kwenye minyororo ya Wazayuni. Larijani amesema kuiunga mkono Palestina ni katika stratijia muhimu za Iran. Ameongeza kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds ni nembo ya azma na irada ya mataifa ya kupigania ukombozi wa Palestina.
Ijumaa Julai Mosi ni Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo watu kutoka matabaka mbalimbali duniani wanatazamiwa kuandamana na kujumuika kwa lengo la kuonesha mfungamano wao na mapambano ya ukombozi wa Palestina sambamba na kuulani utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake.