Sep 22, 2023 02:41 UTC
  • Askofu wa Lebanon: Kuvunjia heshima matukufu ya kidini ni uovu

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiothodoksi la Jabal na Tripoli la Lebanon amelaani vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya kidini na kusisitiza kuwa, kufanya vitendo hivyo ni jambo ovu.

Askofu George Saliba amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la Iran Press mjini Beirut na kueleza kuwa, uhuru wa maoni na kujieleza haipasi kutafsiriwa kama idhini ya kitendo cha kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.

Askofu Saliba ameeleza kuwa: Wanaovunjia heshima matukufu ya kidini hawana dhati ya ubinadamu na wema. Asili yao ni udhalili na chuki dhidi ya watu wengine.

Kiongozi huyo wa Kikristo nchini Lebanon amesema ameghadhabishwa na kukerwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko nchini Sweden na Denmark.

Katika miezi ya hivi karibuni, nchi za Sweden na Denmark zimeshuhudia hujuma na mashambulizi kadhaa dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya kidini, sanjari na kuchomwa moto na kuvunjiwa heshima Kitabu chao kitukufu cha Qur'ani.

Kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden

Huku akitilia mkazo suala la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi pamoja kwa amani na maelewano, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiothodoksi la Jabal na Tripoli la Lebanon amepinga vikali misimamo na mitazamo ya kufurutu mipaka.

Waislamu kote duniani wameendelea kupaza sauti zao kulalamikia vitendo viovu vya kudhalilisha na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Sweden na Denmark, huku kampeni kubwa ya dunia nzima ya kususia bidhaa zinazozalishwa na nchi hizo za Magharibi ikishika kasi.

Tags