Waziri wa Israel yuko Saudia katika ziara ya kwanza ya wazi
Waziri wa Utalii wa utawala wa Kizayuni wa Israel amewasili Riyadh kushiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa, hii ikiwa ni ya ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi ya waziri wa utawala huo haramu nchini Saudi Arabia, kufanyika hadharani.
Haim Katz anaongoza ujumbe wa maafisa wa ngazi ya juu wa utawala haramu wa Israel nchini Saudia, katika ziara ya siku mbili, kwenda kushiriki kile kilichoelezwa kuwa mkutano wa Shirika la Kimataifa la Utalii la Umoja wa Mataifa.
Shirika la habari la al-Jazeera limenukuu taarifa ya Ofisi ya Waziri wa Utalii wa utawala wa Kizayuni wa Israel ikithibitisha habari za safari hiyo. Ofisi hiyo imemnukuu Haim Katz akidai kuwa, "utalii ni daraja baina ya mataifa."
Mamlaka za Saudia hazijatoa taarifa ya kuthibitisha ziara hiyo. Katz amesema, 'Ushirikiano katika uga wa utalii unaweza kuzileta nyoyo pamoja, na ustawi wa kiuchumi."
Waziri wa Utalii wa utawala wa Kizayuni wa Israel ameongeza kuwa, "Nitafanya juu chini kuimarisha ushirikiano, utalii na mahusiano ya kigeni na Israel."
Licha ya kuwa hadi sasa hakuna uhusiano rasmi baina ya Israel na Saudi Arabia, lakini pande hizo mbili hususan kuanzia mwaka 2020, zimechukua hatua katika mkondo wa kupanua wigo wa ushirikiano wao.
Serikali ya Riyadh mwaka jana ilifungua anga yake kwa ajili ya ndege za Israel, na hivi karibuni, irihusu ndege ya Air Sychelles iliyokuwa imebeba abiria 128 wa utawala huo pandikizi kuelekea Tel Aviv, kutua mjini Jeddah eti baada ya kupatwa na hitilafu za kiufundi.
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel mwisho mwa mwezi uliopita alitoa taarifa ya kuishukuru Saudia kwa kuruhusu ndege hiyo itue kwa dharura mjini Jeddah, na kusema kuwa kitendo hicho kimeonyesha ujirani mwema.