Jordan yalaani Wazayuni kuuvamia tena Msikiti wa al-Aqsa
(last modified Wed, 04 Oct 2023 03:08:19 GMT )
Oct 04, 2023 03:08 UTC
  • Jordan yalaani Wazayuni kuuvamia tena Msikiti wa al-Aqsa

Serikali ya Jordan imekosoa vikali hatua ya wanajeshi wa utawala haramu wa Israel kuwashambulia waumini wa Kipalestina, huku mamia ya walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali wakiingia kwa mabavu katika eneo la Msikiti wa al-Aqsa huko Quds (Jerusalem) Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan, Sufyan Qudah ametoa mwito wa kukomeshwa uvamizi huo unaofanywa mara kwa mara na utawala ghasibu wa Isarel dhidi ya Masjidul Aqsa na maeneo mengine matakatifu ya Wapalestina.

Amesema hatua hizo za utawala ghasibu wa Israel hazitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuongeza mizozo, mivutano na vitendo vya utumiaji mabavu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Kundi kubwa la walowezi wa Kizayuni hapo jana waliuvamia tena kwa siku ya nne mtawalia Msikiti wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, huku wakilindwa na kusindikizwa na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Aidha askari wa utawala wa Kizayuni hiyo jana walivamia maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwatia mbaroni raia watano wa Palestina.

Wajordan katika maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina

 

"Israel haina mamlaka juu ya eneo la Quds Mashariki, na wala haina haki ya kuweka vizuizi vya kuingia katika maeneo tukufu," ameeleza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan.

Msikiti wa al-Aqsa unajulikana kuwa nembo kuu ya utambulisho wa Kiislamu na Palestina ya Baitul Muqaddas (Jerusalem) na utawala dhalimu wa Israel unafanya kila njia ili kuifuata athari hiyo muhimu; lakini kusimama imara na kuwa macho wananchi wa Palestina kumeufanya utawala huo ghasibu ugonge mwamba na kushindwa kufikia lengo lake hilo ovu.