Hizbullah: Brigedi za Shahidi Mughniya zimeshambulia vituo vya utawala wa Kizayuni
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza katika taarifa kwamba, Brigedi za Shahidi Imad Mughniya zimeshambulia vituo vitatu vya Wazayuni katika mashamba ya Shab'aa yanayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Taarifa ya Hizbullah imebainisha kuwa, mashambulio hayo yametekelezwa katika mwendelezo wa harakati za kukomboa sehemu iliyosalia ya ardhi ya nchi hiyo inayokaliwa kwa mabavu na vilevile kuonyesha mshikamano na Muqawama wa Wapalestina na watu wa Palestina wapambanaji na wavumilivu.
Jeshi la Kizayuni limetangaza kuwa eneo la Jabel Douf lililoko kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kutokea kusini mwa Lebanon, limelengwa kwa makombora au mizinga.
Kwa mujibu wa mtandao wa Al-Mayadeen, Hizbullah ya Lebanon imetangaza katika taarifa yake kwamba leo asubuhi, Brigedi za Shahidi Imad Mughniya zimeshambulia vituo vitatu vya Wazayuni vya kambi za Radar, Zabdin na Ruwaysat Al-Alam.

Hizbullah ya Lebanon imesisitiza kuwa, shambulio hilo limetekelezwa kwa kutumia idadi kubwa ya makombora ya mizinga na maroketi, na vituo hivyo vimelengwa moja kwa moja.
Kanali ya 14 ya utawala wa Kizayuni imeripoti kuwa kufuatia kufyatuliwa makombora kutoka Lebanon kuelekea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, kamandi ya eneo la kaskazini imetoa amri ya kufungwa vituo vyote vya burudani karibu na mpaka na Lebanon.
Wapiganaji wa Muqawama wa Palestina jana asubuhi walianzisha operesheni ya mashambulio ya pande zote na ya kipekee iliyopewa jina la Kimbunga cha Al-Aqsa kutokea Ukanda wa Gaza dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Operesheni hiyo kubwa na tata ya Muqawama wa Palestina, ambayo ilifanyika kwa kutumia njia za chini ya ardhi, nchi kavu, baharini na angani, pamoja na kurusha maelfu ya maroketi na makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, hadi sasa imepelekea kuangamizwa Wazayuni 300 na kujeruhiwa wengine zaidi ya 1,600.
Kukamatwa mateka askari zaidi ya mia moja wa Kizayuni, miongoni mwao akiwemo jenerali mkuu, na pia kutekwa kwa muda vitongoji saba vya walowezi wa Kizayuni ni miongoni mwa mafanikio mengine ya operesheni hiyo ya kipekee ya Muqawama wa Palestina.
Wakati huohuo gazeti la Independent la Uingereza limethibitisha kuwa Luteni Kanali Jonathan Steinberg, ambaye ni kamanda wa brigedi ya Nahal ya jeshi la utawala wa Kizayuni aliangamizwa katika operesheni iliyotekelezwa jana na Wanamuqawama wa Palestina.../