HAMAS: Kutuma Marekani manowari katika eneo hakuwatishi watu wetu wala Wanamuqawama
Oct 09, 2023 00:05 UTC
Hazem Qassem, msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema: "tangazo la Marekani la kutuma manowari za kubebea ndege za kivita katika eneo hili ni sawa na kushiriki katika uvamizi dhidi ya watu wetu; na ni jaribio la kurejesha morali iliyosambaratika ya jeshi la utawala ghasibu baada ya shambulio la Brigedi za Al-Qassam.
Kwa mujibu wa IRNA; Hazem Qassem ameendelea kueleza kwamba: "harakati hizi haziwatishi watu wetu wala Muqawama wao, na vikosi vya mapambano vitaendelea kuwalinda watu wetu na maeneo yetu matakatifu katika mapigano ya Kimbunga cha Al-Aqsa.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ametangaza kuwa ameliamuru kundi la manowari za kubebea ndege za kivita la Ford lielekee mashariki mwa Mediterania ili kujiandaa kuusaidia utawala dhalimu wa Kizayuni.
Kabla ya hapo Ziad Al-Nakhlah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina alieleza kwamba: utawala wa Kizayuni ulipatiwa msaada na Marekani kuanzia saa za mwanzo kabisa za mashambulizi ya vikosi vya Muqawama wa Palestina.
Al-Nakhlah aliongeza kuwa: "Baraza la mawaziri la adui lazima lisalimu amri mbele ya ukweli huu, na njia ya mkato ya kuepusha kupoteza zaidi askari wao watakaouawa na watakaokamatwa mateka ni kukubali kushindwa."
Tangu siku ya Ijumaamosi, wapiganaji wa Muqawama wa Palestina wameanzisha operesheni yao ya pande zote na isiyo na mfano iitwayo Kimbunga cha Al-Aqsa kutokea Gaza dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu; operesheni ambayo haijawahi kuwa na mfano wake katika historia ya miaka 75 ya utawala bandia wa Israel na kuwapa mshtuko mkubwa Wazayuni.
Operesheni kubwa na ya kushtukiza ya Muqawama wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu inaendelea kwa siku ya tatu, huku vikosi vya makundi mengine ya Muqawama, vikiwemo vya Jihadul-Islami na Arin al-Asud, navyo pia vikiwa vimeungana na wapiganaji wa Hamas, sambamba na Hizbullah ambayo imeshambulia na kuviteketeza vituo vitatu vya udukuzi na rada vya utawala wa Kizayuni katika eneo unalolikalia kwa mabavu la Shab'aa kusini mwa Lebanon.../