Wamarekani 3 wauawa katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa
Shirika la habari la CNN limetangaza kuwa takriban raia 3 wa Marekani wameuawa katika operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.
CNN imeongeza kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inafahamu kuhusu vifo vya raia wake watatu huko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel, karibu na Ukanda wa Gaza, pamoja na Wamarekani wengine ambao hawajulikani waliko.
Inasemekana pia kwamba ubalozi wa Marekani huko Beitul Muqaddas umesasisha mipango yake ya dharura ya uwezekano kuwaondoa raia wake Israel kupitia safari za nchi kavu au za anga.
Wapiganaji wa muqawama wa Palestina wameanzisha operesheni kali, ya pande zote na ya kipekee inayoitwa Kimbunga cha al-Aqsa kutokea Gaza (kusini) dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu tangu Jumamosi asubuhi. Operesheni hiyo ambayo imewashtua maghasibu wa Kizayuni haijawahi kutokea katika historia ya miaka 75 ya kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina.
Operesheni hiyo kubwa ya muqawama wa Palestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu inaendelea katika siku yake ya tatu, huku vikosi vya makundi mengine ya muqawama, kama Jihad Islami na Arin al-Usud, navyo vikiungana na wapiganaji wa Hamas. Hizbullah ya Lebanon pia imeshambulia na kuharibu vituo vitatu vya kijeshi vya Wazayuni katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Shabaa kusini mwa Lebanon.