Hamas: Tunalenga jeshi vamizi la Israel, hatushambulii raia na watoto
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i103342-hamas_tunalenga_jeshi_vamizi_la_israel_hatushambulii_raia_na_watoto
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza leo Jumatano kwamba wanamapambano wa Palestina na wapiganaji wa tawi lake la kijeshi, Brigedi za Al-Qassam, wanaepuka raia, na wanalenga tu mfumo wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2023 08:31 UTC
  • Hamas: Tunalenga jeshi vamizi la Israel, hatushambulii raia na watoto

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetangaza leo Jumatano kwamba wanamapambano wa Palestina na wapiganaji wa tawi lake la kijeshi, Brigedi za Al-Qassam, wanaepuka raia, na wanalenga tu mfumo wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Operesheni Kimbunga cha Al-Aqsa.

Taarifa iliyotolewa na Hamas imekanusha madai yanayotolewa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kwamba wapiganaji wake wanalenga watoto, ikitoa wito kwa vyombo hivyo vya habari kuwa makini na kutoegemea upande wa Wazayuni.

Hamas imesema kwamba, hatua ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi ya kuripoti madai kwamba harakati hiyo imeua watoto wachanga, kuwakata vichwa na kuwalenga raia ni "uongo na mporomoko wa vyombo vya habari katika jaribio la kuficha jinai na mauaji ya utawala vamizi yanayofanywa mchana na usiku huko Gaza. Hamas imesema, mauaji yanayofanywa na Israel ni uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki kutokana na kuwalenga raia na kuwakatia umeme, maji, chakula na huduma za matibabu.”

Taarifa ya Hamas imeeleza kuwa: Wapiganaji wake wanalenga mfumo wa jeshi na usalama wa utawala wa Kizayuni katika vita vya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, ambavyo ni shabaha halali, na wakati huo huo wanajitahidi kuepuka maeneo ya raia. Imesema, picha na video za mahojiano ya baadhi ya walowezi wa Kizayuni zinakadhibisha riwaya ya propaganda chafu inayosambazwa katika vyombo vya habari vya Magharibi.

Taarifa ya Hamas imetolewa baada ya madai kwamba wanachama wa Brigedi ya Al-Qassam, tawi la kijeshi la harakati ya Hamas, "waliwakata vichwa watoto wengi wa Israeli" wakati wa shambulio la Oktoba 7, na madai haya yamepigiwa debe katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi.

Sambamba na hayo ofisi ya msemaji wa jeshi la Israel ilisema jana, Jumanne, kwamba haikuwa na taarifa zozote za kuthibitisha madai hayo yaliyochapishwa katika magazeti ya Israel na kuenea kwenye mitandao ya kijamii.